RAIS WA BENKI YA BIASHARA NA MAENDELEO AIPONGEZA TANZANIA KWA KUJENGA RELI YA KISASA

  • Rais na Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Dkt. Admassu Tadesse ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR) kwa kutumia fedha zake za ndani na kuahidi kuwa Benki yake itafanya kila linalowezekana kuhakikisha inatafuta fedha za kujenga reli hiyo
  • Dkt. Tadesse ametoa kauli hiyo alipotembelea sehemu ya ujenzi wa miundombinu ya reli hiyo, kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro na kujionea kazi kubwa iliyofanyika ambapo amesema mradi huo hautainufaisha Tanzania peke yake bali pia nchi za ukanda wa Afrika hususan ambazo hazipakani na Bahari.
  • Kiongozi huyo wa juu wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Dkt. Tadesse, ameeleza kuwa mwaka huu Benki yake imeipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani bilioni moja sawa na takribani sh. za Tanzania trilioni 2.3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yake mikubwa ya maendeleo.
  • Ameongeza kuwa Tanzania imenufaika pia na kiasi kingine cha zaidi ya dola za Marekani bilioni moja zilizotolewa na Benki yake miaka ya nyuma na ameelezea kufurahishwa kwake na namna nchi inavyokua kwa kasi kiuchumi na kwamba inakopesheka.
  • Aliahidi kuwa kwa kuwa fedha zinazohitajika kukamilisha ujenzi wa mradi huo wa reli ya kisasa ni nyingi, Benki yake itazishawishi taasisi nyingine za fedha ndani na nje ya Bara la Afrika kuchangia ujenzi huo ili mradi ukamilike kwa wakati ili kuchochea masuala ya Bashara na kuboresha shughuli za usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo.
  • Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Bw. Masanja Kadogosa, ameishukuru Benki hiyo kwa kuonesha nia ya kusaidia ujenzi wa Reli hiyo katika awamu zinazofuata.
  • Alisema kuwa mpaka sasa ujenzi wa Reli ya Kisasa ambao umetumia fedha za ndani kati ya Dar es Salaam hadi Morogoro umekamilika kwa asilimia 72 huku kipande cha Morogoro hadi Makutupora mkoani Singida kikiwa kimekamilika kwa asilimia 22.
  • Bw. Kadogosa amesema kuwa Serikali inatafuta fedha nyingine kwa ajili ya kujenga reli hiyo  kuanzia Makutupora, Tabora, Isaka hadi Mwanza na kwamba watafanya mazungumzo na Benki hiyo kuona namna watakavyofadhili ujenzi huo. Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Ad

Unaweza kuangalia pia

WAKAZI WA PEMBEZONI MWA BAHARI WAELIMISHWA ATHARI ZA MAGENDO

Wakazi na wafanyabiashara waishio pembezoni mwa fukwe za Bahari ya Hindi katika kata za Somangila, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *