JAPAN YAAHIDI KUENDELEA KUSAIDIA MAENDELEO YA TANZANIA

  • Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameiomba Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA) kusaidia upatikanaji wa fedha kwa njia ya mikopo nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ikiwemo reli ya kisasa, nishati na kilimo.
11-01
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akisikiliza maelezo kutoka kwa mgeni wake, Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA) Dkt. Nobuko Kayashima (hayupo pichani) walipokutana Jijini Dodoma ambapo Japan imeahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika Nyanja mbalimbali za maendeleo.
  • Dkt. Mpango ametoa maombi hayo Jijini Dodoma, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa JICA, Dkt. Nobuko Kayashima, ambapo wawili hao wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa miradi inayokusudiwa kufadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika hilo.
22-01
Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA) Dkt. Nobuko Kayashima akisisitiza jambo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) Jijini Dodoma ambapo JICA imeahidi kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania.
    • Amesema kuwa hivi sasa Serikali imeelekeza nguvu na  fedha zake za ndani kujenga Reli kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), Ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme kwa njia ya maporomoko ya maji ya Mto Rufiji mkoani Pwani (Nyerere Hydral Power Plant), na kwamba miradi  inahitaji fedha nyingi ambazo anaamini Japan inaweza kusaidia upatikanaji wake.

  • “Tumeanza kutekeleza miradi hii kwa kutumia fedha zetu za ndani na tunaiomba Serikali ya Japan kuzishawishi taasisi zake za fedha kwa kushirikiana na taasisi nyingine kutupatia mikopo yenye masharti nafuu ili tuweze kukamilisha miradi hiyo muhimu kwa Taifa” alisema Dkt. Mpango
33-01
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akiwa katika picha na mgeni wake, Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA) Dkt. Nobuko Kayashima walipokutana Jijini Dodoma ambapo Japan imeahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika Nyanja mbalimbali za maendeleo.
  • Alifafanua kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza shughuli za kiuchumi na kibiashara hapa nchini pamoja na nchi jirani ambazo hazijapakana na Bahari huku nishati ya umeme ikitarajiwa kuboresha upatikanaji wa umeme kwa ajili ya kuendesha reli hiyo pamoja viwanda.
  • Aidha, Dkt. Mpango amemwomba kiongozi huyo wa JICA kusaidia Wizara na Serikali kwa ujumla kuendeleza rasilimali watu ama nguvu kazi kwa kuwapatia fursa ya masomo nchini Japan wataalam kutoka Wizara yake na maeneo mengine serikalini ili kuongeza ubobezi wa wataalam hao katika sekta ya uchumi, fedha, pamoja na tiba hususan matibabu ya moyo na figo.
55-01
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa tano kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na mgeni wake, Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA) Dkt. Nobuko Kayashima (wa tano kulia), pamoja maafisa wengine waandamizi kutoka JICA, Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Uchukuzi baada ya mazungumzo yaliyofanyika Jijini Dodoma kati ya pande hizo mbili.
  • “Pia ninaliomba Shirika lako lisaidie kuboresha miundombinu ya barabara za kuzunguka Jiji la Dodoma kutokana na mahitaji makubwa baada ya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi, pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nsalato-Dodoma” aliongeza Dkt Mpango
  • Alisema kuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa-Msalato unahitaji kujengwa njia ya kuruka na kutua ndege pamoja na ujenzi wa majengo ya abiria.
77-01
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akiteta jambo na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adolf Ndunguru nje ya Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha na Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA) Dkt. Nobuko Kayashima.
  • “ Pia nimewaomba wenzetu ambao wanauzoefu mkubwa watusaidie katika kilimo cha mpunga na nimetoa mfano wa Bonde la Ruvu ambalo ni kubwa na lina fursa ya kuzalisha mchele wa kutosheleza mahitaji ya ndani na nje na tukichagua eneo moja na kulitumia vizuri tutamaliza mahitaji ya mchele katika Taifa letu” alisisitiza Dkt. Mpango
  • Akijibu maombi ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Makamu huyo wa Rais wa JICA, Dkt. Nobuko Kayashima, alikubali maombi ya kusaidia kuendeleza rasilimali watu ambapo kwa kuanzia Shirika hilo limeahidi kutoa nafasi ya watumishi 15 kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na  Sekta nyingine kupata ufadhili wa masomo nchini Japan.
88-01
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati) akiagana na mgeni wake, Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA) Dkt. Nobuko Kayashima (kulia) pamoja na kurugenzi Msaidizi wa JICA, Bi. Yuriko Doi, nje ya jengo la Treasury Square, Jijini Dodoma. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
  • Amesema Serikali ya Japan kupitia Shirika lake litaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi ambapo miradi mipya inayokusudiwa kufadhiliwa na Shirika lake ni Mradi wa Upanuzi wa Bandari ya Kigoma, Ujenzi wa Barabara ya Arusha-Holili na Mradi wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Zanzibar.
  • Kuhusu uendelezaji wa kilimo, Dkt. Kayashima ameahidi kuwa Shirika lake litaendelea kujihusisha na kuendeleza zao la mpunga hapa nchini ili kuwasaidia wakulima kujikimu kimaisha pamoja na kusaidia nchi ijitosheleze kwa chakula
Ad

Unaweza kuangalia pia

WAKAZI WA PEMBEZONI MWA BAHARI WAELIMISHWA ATHARI ZA MAGENDO

Wakazi na wafanyabiashara waishio pembezoni mwa fukwe za Bahari ya Hindi katika kata za Somangila, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *