SERIKALI YAWAFUTA MACHOZI WAKAZI WA KATA YA SUNYA

NA SAKINA ABDULMASOUD,KITETO.

“Siku moja nilimshuhudia mama mmoja alikuwa mjamzito,alianza kuumwa tukataka kumpeleka hospitali,tulihangaika usafiri kwa watu mpaka tunakuja kuupata yule mama alishahangaika sana kwa uchungu,lakini tunamshukuru Mungu tulimfikisha na alijifungua salama,”ni Sefae Zibani mkazi wa Kata ya Sunya mkoani Manyara.

Ad

Mkazi huyo na wenzake wanarudisha nyuma kumbukumbu wakati wakitembea umbali wa kilomita 125 kufuata huduma za afya katika hospitali ya wilaya ya Kiteto au kulazimika kwenda kupata huduma hiyo wilayani Kilindi mkoani Tanga ambapo wanapakana napo.

Kwa mujibu wa wakazi hao wanasema umbali huo ulisababisha pia akina mama wajawazito kupoteza maisha baada ya kukosa huduma kwa haraka.

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, TAMISEMI Selemani Jafo akitoa maelekezo baada ya kukagua kituo cha afya cha Sunya kilichopo wilayani Kiteto,miongoni mwake yupo mbunge wa jimbo la Kiteto Emmanuel Papian na mkuu wa wilaya hiyo Tumaini Magessa.

“Nilikuwa namuomba Mungu nisije kupata ujauzito kwa sasa,maana changamoto niliyokuwa naiona haikunipa amani ya mimi kutaka kushika ujauzito,”alisema Theresia Luizo mkazi wa Sunya.

Waswahili wanasema kilio kina mwenyewe,vilio hivyo vinapata majibu baada ya serikali kujenga kituo cha afya katika kata hiyo ambacho kitakuwa na huduma zote muhimu na hivyo kuwafuta machozi akina mama waliolia muda mrefu,lakini pia kuwaondolea woga na hatimaye kufikiria suala la kubeba ujauzito.

Mei 14 mwaka huu,Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)Selemani Jafo anafika kuzindua kituo hicho kinachotarajiwa kutoa huduma kwa wakazi 38,273 wa kata hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Kiteto Tumaini Magessa anasema kituo hicho kimekamilika,kimeanza kutoa huduma na kubainisha changamoto zilizopo ikiwemo ukosefu wa umeme.

“Kutokana na changamoto hii kwa sasa tunalazimika kutumia jenereta,ila Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani alishafika hapa,tumemuelezea na ameahidi kutuletea umeme,”alisema mkuu huyo.

Anasema wilaya hiyo ina tarafa saba na ili kuhudumia wananchi wengi zaidi wanaomba kuongezewa vituo viwili vya afya kutokana na wilaya hiyo kutawanyika.

Akitoa taarifa ya ujenzi huo Mkurugenzi wa halmashauri ya Kiteto Tamimu Kambona anasema ujenzi huo ulianza januari 2018 na umekamilika mwaka 2019 kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 510 ambapo kiasi cha Sh milioni 483.4  zimetumika na kiasi cha Sh milioni 35 ni bakaa ambazo zitatumika kwa ajili ya kujenga duka la dawa.

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,TAMISEMI Selemani Jafo akifafanua jambo baada ya kuzindua kituo cha afya cha Sunya kilichopo wilayani Kiteto Mkoani Manyara.

“Uwepo wa kituo hiki utasaidia kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu waliyokuwa wanapata wananchi pindi walipotaka huduma za afya lakini pia kutapunguza vifo vya mama wajawazito na watoto,”alisema mkurugenzi.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo mbunge wa Kiteto Emmanuel Papian kwa niaba ya wananchi anaishukuru serikali kwa kukamilisha kituo hicho na kumuomba waziri afikishe salamu zao kwa Rais Dkt John Magufuli.

“Mheshimiwa Waziri sisi wana Kiteto tulishamaliza uchaguzi zamani na kura zetu zote tumeshazipeleka kwa dkt Magufuli ili awe Rais tena kwa kipindi cha mwaka 2020/2025,tunachoomba aje tumshukuru kwa kazi aliyotufanyia maana matatizo yetu alishayamaliza kuyatatua,’alisema mbunge huyo.

MAAGIZO YA WAZIRI JAFO.

Akizindua kituo hicho Jafo anawataka wataalam wa afya kujipanga katika  kutoa huduma nzuri inayotarajiwa.

Aidha anawataka wananchi kuhakikisha wanalinda miundombinu ya kituo hicho ili dhamira ya serikali iliyopo ya kusogeza huduma za afya karibu na wananchi iweze kutimia .

 “Changamoto mojawapo ilikuwa ni ukosefu wa kituo cha afya na hivyo kulazimu wananchi kwenda wilayani Kilindi mkoani Tanga au kusafiri kilomita 125 kufuata huduma katika hospitali ya wilaya,”alisema Jafo.

Anasema kituo hicho ni miongoni mwa vituo vilivyopewa kiasi cha Sh milioni 400 na ujenzi umekamilika kwa kiwango alichoridhika nacho.

“Niwaombe wananchi mshirikiane katika kutunza miundombinu ya kituo hiki,sitarajii nikija hapa nikute mmeharibu koki hapana,kila mtu awe mlinzi wa mwenzake ili kituo hiki kiwe na manufaa kwa sisi na vizazi vyetu vijavyo,”alisisitiza Jafo.

MIPANGO YA SERIKALI 2020/2021.

Yote hayo yanafanyika ikiwa ni kutimiza dhamira serikali ya awamu ya tano iliyotokana na ahadi zilizopo katika Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Katika ilani hiyo serikali imeahidi kuendeleza utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa afya ya msingi(MMAM)weye lengo la kuimarisha na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa kuhakikisha kila kijiji kina kuwa na zahanati,kata inakuwa na kituo cha afya na wilaya kuwa na hospitali.

Na ikiwa sasa ni bajeti ya mwisho ya awamu ya kwanza ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt Magufuli serikali imepanga kujenga wodi tatu katika kila halmashauri na ujenzi wa hospitali 27 za halmashauri.

Akiwasilisha bajeti hiyo hivi karibuni bungeni jijini Dodoma,Jafo anasema wodi hizo tatu katikak ila hospitali za halmashauri zitanufaisha hospitali  67 za halmashauri ambazo zinaendelea kujengwa na zimetengewa Sh bilioni 32.50 kwa ajili ya kazi hiyo na Sh bilioni 27.00 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya 27 za halmashauri.

“Ili kukamilisha ujenzi wa zahanati tatu katika kila halmashauri zimetengwa jumla ya Sh bilioni 27.75 na kipaumbele kitakuwa ni  ni kukamilisha maboma ya zahanati zilizoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi na pia itafanyika ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali 67 za halmashauri ambapo Sh bilioni 32.50 zimetengwa,”anasema Jafo.

Akizungumzia mpango wa uimarishaji wa huduma za afya ya msingi kwa matokeo anasema zimetengwa Sh bilioni 128.91 kwa ajili ya ukamilishaji wa vituo vya afya,ununuzi wa vifaa tiba,ajira za watumishi wa afya kwa mkataba,kujenga uwezo wa watumishi na usimamizi wa mradi.

Anasema yote yanafanyika ili kuziwezesha hospitali hizo na vituo vya afya kuanza kutoa huduma na kutimiza lengo na dhamira ya serikali ya awamu ya tano.

Ad

Unaweza kuangalia pia

“Tusikubali Kuwa Tarumbeta za Watu Wasio Tutakia Mema”

“Tusikubali kuwa tarumbeta za Watu wasio tutakia mema, Maadili Yetu Mazuri Ya Kitanzania Lazima Tuyatunze, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *