RAIS MAGUFULI ASHUHUDIA UZINDUZI WA MSIKITI, CHAMWINO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 26 Oktoba, 2020 ameshuhudia uzinduzi wa Msikiti wa Sheikh Abubakar Zubeir Ally uliojengwa Chamwino Mkoani Dodoma kwa gharama ya shilingi Milioni 319.3 zilizotokana na michango ya viongozi, taasisi na watu mbalimbali.

Ujenzi wa Msikiti huo ulianza tarehe 28 Agosti, 2020 ikiwa ni siku 3 baada ya Mhe. Rais Magufuli kuitisha harambee ya kuchangisha fedha za kujenga Msikiti mpya kwa ajili ya Waislamu wa Chamwino, akiwa katika Ibada ya uzinduzi wa Kanisa Katoliki la Bikira Maria Imakulata Ikulu-Chamwino ambalo pia limejengwa kwa harambee iliyoendeshwa na Mhe. Rais Magufuli.

Ad
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimsaidia Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally kufungua rasmi msikiti wa Chamwino Ikulu mkoani Dodoma leo Oktoba 26, 2020. Msikiti huo umepewa jina la Sheikh Abubakar Zubeiry bin Ally

Uzinduzi wa Msikiti huo umefanywa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Ally ambapo pamoja na Mhe. Rais Magufuli, sherehe za uzinduzi huo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Madhehebu mbalimbali ya Dini, viongozi wa taasisi, na watu mbalimbali waliochangia ujenzi huo.

Mkuu wa JKT Mej. Jen. Charles Mbuge amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuiamini JKT kujenga miradi mbalimbali na amesema kutokana na Msikiti huo kujengwa na JKT gharama za ujenzi zimekuwa shilingi Milioni 319.3 ikilinganishwa na shilingi Milioni 439.4 kama ujenzi ungefanywa na kampuni za ukandarasi.

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir Ally amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa moyo wake wa upendo na ucha Mungu wake uliomuongoza kuchangisha fedha zilizofanikisha kujengwa kwa Msikiti huo, pamoja na Msikiti mkubwa wa kimataifa uliojengwa Kinondoni Jijini Dar es Salaam ambapo Mhe. Rais Magufuli alimuomba Mfalme Mohammed VI wa Morocco kufadhili ujenzi huo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimsaidia Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally kukata utepe kufungua rasmi msikiti wa Chamwino Ikulu mkoani Dodoma leo Oktoba 26, 2020. Msikiti huo umepewa jina la Sheikh Abubakar Zubeiry bin Ally

Sheikh Abubakar Zubeir Ally pia amezishukuru taasisi na watu wote waliojitokeza kuchangia ujenzi huo na ameongoza Dua ya kuuombea Msikiti, Taifa la Tanzania na uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika sherehe za uzinduzi wa Msikiti huo, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania kwa kukubali harambee ya kuchangia ujenzi wa Msikiti huo, amezishukuru taasisi na watu mbalimbali waliojitokeza kumuunga mkono kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi huo na ameipongeza JKT na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kujenga Msikiti mzuri, imara na kwa muda mfupi.

Mhe. Rais Magufuli amesema anaamini kuwa kujengwa kwa Msikiti huo sio tu kutawafaa Waislamu watakaoutumia kuswali bali pia utadumisha amani, upendo na umoja wa Watanzania.

Taswira ya juu ya msikiti mpya wa Chamwino Dodoma ambao umepewa jina la Sheikh Abubakary Zubeiry Ally, Mufti Mkuu wa Tanzania kwenye hafla fupi iliyohudhuriwa na JPM leo Jumatatu Oktoba 26, 2020

Amesisitiza kuwa baada ya kukamilisha ujenzi huo anadhamiria kufanya harambee nyingine ya kuchangisha fedha kwa ajili Dhehebu la Dini linalofanya Ibada ya Juma siku ya Jumamosi na ameeleza kuwa atafurahi kuona Ikulu ya Chamwino ikiwa imezungukwa na Makanisa na Misikiti.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Mitazamo ya Uongozi ya Mhe. Ummy Ally Mwalimu katika Sekta za Afya, Maendeleo ya Jamii, na Haki za Watoto

Ummy Ally Mwalimu ameonyesha mitazamo ya uongozi yenye mwelekeo wa kujali maendeleo na ustawi katika …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *