Katibu Mtendaji wa Sekretariet ya SADC Dkt. Stergomena L. Tax na Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Bw. Laurean Rugambwa Bwanakunu wamesaini mkataba wa makubaliano ya MSD kuwa mnunuzi Mkuu wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwa ajili ya nchi 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Hatua hii inafuatia uteuzi wa serikali ya Tanzania kupitia Bohari ya Dawa (MSD) ulifanywa wakati wa mkutano wa SADC wa mawaziri wa Afya wa nchi wanachama, uliofanyika mwezi Novemba, 2017 nchini Afrika Kusini.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Bw. Laurean Bwanakunu amesema tangu wakati huo hadi sasa wamekuwa wakishirikiana na na Sekretarieti ya (SADC) kuandaa rasimu ya mpango wa utekelezaji wa manunuzi ya pamoja yaani SADC Pooled Procurement Services (SPPS).
Amesema kulingana na mpango huo, uratibu wa manunuzi unaanza rasmi tarehe leo, tarehe 9/10/2018, kupitia mkataba wa makubaliano yaani Memorandum of Understanding (MoU) kati ya MSD na Sekretarieti ya SADC.
Bwanakunu ameongeza kuwa MSD itakuwa na majukumu ya kupokea mahitaji ya manunuzi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kutoka kwa nchi hizo 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara, kusimamia takwimu na taarifa za dawa pamoja na kusimamia Kanzidata (Database) ya dawa za nchi hizo.
Ameongeza kuwa MSD itasimamia bei elekezi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara, kusimamia mfumo wa manunuzi kwa njia ya mtandao kwa nchi zote wanachama, kutoa huduma za kitaalam na kupanga bei elekezi.
MSD pia itaanzisha kitengo maalumu ndani ya kurugenzi ya manunuzi kwa ajili ya kazi hii ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba ba vitendanishi vya maabara kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya SADC tu.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Sekretariet ya SADC Dkt. Stergomena L. Tax ameeleza kuwa Tanzania kuwa mnunuzi mkuu wa dawa kwa nchi za Ukanda wa SADC ni heshima kubwa kwa Taifa, kuaminiwa kwa huduma bora, uwezo na kukidhi vigezo vya kitaalamu katika mnyororo wa ugavi.
Makubaliano hayo yameshuhudiwa na Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye amesema kwamba SADC imeipa Tanzania heshima kubwa na kuichagiza MSD kuhakikisha inatekeleza majukumu yake vizuri ili isionekane kuwa SADC ilifanya makosa kuichagua Tanzania.
#SisiNiTanzaniaMpyA+