- Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ameliagiza Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuongeza ukubwa wa transifoma kutoka 100kV hadi kufikia 200kV katika kijiji cha Mwamashimba wilayani Igunga mkoani Tabora kutoka mahitaji makubwa ya umeme.
- Mgalu alitoa maagizo hayo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa usambazaji na kuwasha huduma ya umeme vijijini kupitia mradi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa 400kV Backbone (BTIP) katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora pamoja na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa REA III awamu ya kwanza.
- Mgalu alitoa maagizo hayo katika Kijiji cha Mwamashimba chenye mahitaji makubwa ya umeme baada ya wanakijiji wengi kuanzisha viwanda vidogodogo zikiwemo mashine za kusaga na kukoboa nafaka, mashine za kukamua mafuta yatokanayo na mbegu pamoja kuwepo kwa shughuli nyingi za uchomeleaji vyuma.
- “Hapa Mwamashimba kunahitajika umeme zaidi maana watu wamejiajiri kwelikweli, wanafanya shughuli za maendeleo, hii ndiyo sera ya Serikali ya awamu ya tano, kwamba umeme uwafikie wananchi na uwanufaishe kwa kubadili maisha yao,transifoma mliofunga haiKidhi shughuli zao ni nyingi mnooo, TANESCO, hakikisheni mnaongeza transfoma nyingi walau wawe wanapata umeme wa 200kV, kutoka 100kV ya sasa, ili wahamasishe na vijiji vingine”, alisema Mgalu.
- Katika ziara hiyo, Mgalu aliwataka wananchi waliopitiwa na mradi wa BTIP kujiandaa kwa kusuka nyaya katika nyumba zao ili mkandarasi anapopita katika maeneo yao wawe tayari kuunganishwa na huduma hiyo kwa bei nafuu ya 27,000.
- Aidha aliwatoa hofu wananchi wote wa maeneo husika kuwa watapata huduma ya umeme kwa kuwa tayari wakandarasi wamefanya upimaji na kuwa na ramani ya utekelezaji, usambazaji na uunganishaji wa umeme katika Vijiji vyote vilivyopitiwa na BTIP.
- Amewaasa wananchi kuendelea kutunza na kuilinda miundombinu ya umeme zikiwemo nguzo kwa kutoichoma moto, kutoiba vifaa mbalimbali ya miundombinu hiyo pamoja na kulima kwa njia salama katika majaruba.
- Sambamba na hilo aliwataka wananchi hao pamoja na wakandarasi kushirikiana pamoja katika kutekeleza mradi huo katika maeneo yao, pia wananchi wa eneo husika wapatie fursa ya ajira kulingana na uwezo wao wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
- Akiwa wilayani humo, Mgalu aliwasha huduma ya umeme katika vijiji vya Mwabakima ambapo 120 wanatarajia kunufaika kwa kuunganishwa huduma ya umeme katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa BTIP , wateja 35 kati yao tayari wameunganishwa na huduma hiyo, Vilevile aliwasha huduma ya umeme katika kijiji cha Mwashimba ambapo wateja 150 wataunganishwa na huduma ya umeme katika awamu ya kwanza, 40 kati yao tayari wameshaunganishwa na huduma hiyo.
- Katika kijiji cha Jogohya, Mgalu alikagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo na kumtaka mkandarasi kutoka kampuni ya OK, kuharakisha kazi ya kujenga miundombinu kwa kuwa wananchi wengine wamekuwa wakiusubiri mradi huo kwa shauku kubwaa.
- Katika hatua nyingine ,Naibu waziri huyo aliwataka wazazi, viongozi wa Serikali za mitaa pamoja vijijini, walimu pamoja na wakazi wa vijiji hivyo vya wilaya ya Igunga kuhakikisha wanapiga marufuku, wanapinga na kukataa kabisa ndoa za umri mdogo na mimba kwa watoto wadogo hasa wanafunzi.
Ad