Wananchi wa Kijiji cha Musanja, Kata ya Musanja wamejitolea kwa hali na mali kujenga daraja linalounganisha Vitongoji vya Kaharaga na Kukema (ilipo S/M Musanja) ili kurahisisha mawasiliano kati ya Shule na Jamii inayozunguka Shule hiyo.
Ujenzi wa Daraja hilo utasaidia wanafunzi wanaosoma shule ya msingi Musanja waliokuwa wanapata shida ya kufika shule kipindi cha mvua kutokana na kushindwa kuvuka katika eneo hilo.Aidha daraja hilo linajengwa kwa kwa ushirikiano wa wananchi wa eneo hilo na walio nje ya kijiji cha Musanja kwa kuchangia fedha za ujenzi.
Awali, akizungumza na Mwandishi wa Habari hizi, Afisa Mtendaji wa Kijiji, Ndugu Emmanuel Eswaga alisema, “Hadi kukamilika kwa ujenzi huo, Jumla ya Tsh Milioni 15.9 zinahitajika ikiwa ni gharama za Mchanga, Mawe, Saruji, Nondo, Kokoto na Malipo ya Fundi.”
Amesema kuwa katika gharama hizo wananchi wa Kijiji cha Musanja wamebeba jukumu la kusomba mchanga, mawe, maji na kokoto,kwa upande wake Mbunge wa Jimbo Prof Sospeter Muhongo amesema kuwa atakwenda kutembelea mradio huo na kutoa mchango wake katika kusaidia wananchi hao walijitolea.