SIMIYU: Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Bw. Anthony Mtaka

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 08 Septemba, 2018 ameendelea na ziara yake katika Kanda ya Ziwa ambapo ameweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Lamadi na kufungua barabara za Mji wa Lamadi katika Wilaya ya Busega, amefungua jengo la wagonjwa wa nje (OPD) la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, na ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Maswa – Bariadi.

Mradi wa maji wa Lamadi utakaozalisha lita Milioni 3.3 za maji kwa siku ambayo ni mara mbili ya mahitaji ya lita Milioni 1.8 ya wakazi wa mji huo kwa sasa, utatatua kero ya miaka mingi ya uhaba wa maji kwa wakazi hao ambao kwa sasa wanapata maji kwa asilimia 23 tu ya mahitaji yao.

Ad

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa mradi huo ambao umepangwa kukamilika mwezi Mei 2019 utagharimu shilingi Bilioni 12.83 na ni sehemu ya mpango wa uboreshaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira wa ziwa Victoria (LV WATSAN) unaotekelezwa katika miji ya Mwanza, Musoma, Bukoba, Magu, Misungwi na Lamadi kwa gharama ya shilingi Bilioni 276, fedha ambazo zimetolewa kwa mkopo nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Serikali ya Tanzania.

Screen Shot 2018-09-08 at 9.11.21 PM.png

Ujenzi wa barabara za Mji wa Lamadi zenye jumla ya kilometa 6.26 umegharimu shilingi Bilioni 9.192 ambapo barabara hizo zimewekewa taa, mifereji, njia za waenda kwa miguu na eneo la kuegesha magari lenye ukubwa wa meta 900.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa pamoja na barabara hizo Serikali itajenga kituo cha mabasi na kilometa nyingine 1.5 ya barabara, kununua gari la taka na kuandaa ramani ya mpango mji katika Mji wa Lamadi kwa gharama ya shilingi Bilioni 6.47, na kwamba mradi kama huo unatekelezwa katika miji mingine 17 hapa nchini kwa gharama ya shilingi Bilioni 561 ikiwa ni fedha za mkopo nafuu ktoka Benki ya Dunia.

Jengo la wagonjwa wa nje la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu limejengwa katika eneo la Nyaumata kwa ghamara ya shilingi Bilioni 1.8, na ni sehemu ya mradi mzima wa ujenzi wa miundombinu ya hospitali hiyo uliopangwa kugharimu shilingi Bilioni 11. Gharama za ujenzi huo zimepungua kutoka makadirio ya awali ya shilingi Bilioni 46 baada ya Mhe. Rais Magufuli kutembelea mradi huo mwaka juzi na kutoa maelekezo ya kutaka zipunguzwe ili ziendane na gharama halisi za ujenzi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali imetenga shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kujenga miundombinu mingine ya hospitali hiyo katika kipindi cha miezi 6, na kwa kuunga mkono ukamilishaji wa haraka wa hospitali hiyo Mhe. Rais Magufuli ameahidi kuongeza fedha nyingine shilingi Bilioni 4.

Ujenzi wa barabara ya Maswa – Bariadi yenye urefu wa kilometa 49.7 utagharimu shilingi Bilioni 88.877, na barabara hii ni sehemu ya barabara ya Mwigumbi – Maswa – Bariadi – Lamadi yenye urefu wa kilometa 171.8.

Akizungumza katika miradi hiyo Mhe. Rais Magufuli amezishukuru taasisi zote za kimataifa zilizotoa mikopo nafuu kwa Tanzania kwa lengo la kufanikisha miradi hiyo, na ameahidi kuwa Serikali itahakikisha miradi hiyo inatekelezwa vizuri na inaleta manufaa yanayotarajiwa kwa wananchi.

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Simiyu kwa kupata miradi hiyo na ametoa wito kwa Watanzania wote kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuwaletea maendeleo, ikiwa ni pamoja na kulipa kodi kwa kuwa fedha za kugharamia miradi hiyo zinatokana na kodi zao.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Bw. Anthony Mtaka, viongozi na wakulima wa mkoa wa Simiyu kwa juhudi kubwa walizofanya katika kuongeza uzalishaji wa zao la pamba, ambapo katika msimu uliopita kati ya kilo Milioni 226 zilizozalishwa hapa nchini, kilo Milioni 120 zimezalishwa katika Mkoa wa Simiyu.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha haraka ujenzi wa miundombinu ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu.

Mhe. Rais Magufuli pia ameagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji kuhakikisha fedha za vijana na wanawake (asilimia 10) zinatengwa kama inavyopaswa ili kuwawezesha vijana kupata fedha za kufanya shughuli za ujasiriamali.

Mhe. Rais Magufuli kesho anaendelea na ziara yake hapa Mkoani Simiyu kwa kutembelea Wilaya ya Meatu.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Bariadi

08 Septemba, 2018

Ad

Unaweza kuangalia pia

ONGEZENI KASI YA KUWAHUDUMIA WANANCHI – DKT. CHAULA

Watumishi wa afya nchini wametakiwa kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi kwenye vituo vya kutolea huduma …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *