- Aagiza vijiji vyenye shida ya maji Bumbuli vibainishwe
- Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha wananchi katika vijiji vyote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama katika jimbo la Bumbuli.
- Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Bumbuli, wilayani Lushoto, Charles Boy afanye utafiti na kubainisha vijiji vyenye shida ya maji Bumbuli.
- Amesema baada ya kuvibaini vijiji hivyo, anatakiwa aweke mpango wa kuhakikisha navyo vinapata huduma ya maji safi ili kuwaondolea wananchi tatizo hilo la ukosefu wa maji.

- Alitoa agizo hilo jana jioni wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mponde jimbo la Bumbuli, Lushoto.
- Waziri Mkuu ambaye jana alihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tanga, aliwapongeza wakazi wa wilaya ya Lushoto kwa kutunza mazingira na vyanzo vya maji.
- Alisema Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote yenye changamoto hiyo nchini.
- “Serikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama.”
- Waziri Mkuu aliongeza kuwa upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali, hivyo aliwataka wananchi waendelee kuiamini Serikali yao.
- Awali, Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi, ukarabati wa miradi ya maji, ambapo mkoa wa Tanga umetengewa sh. bilioni 13.
- Aweso alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa wakandarasi wanajenga miradi ya maji wazingatie viwango vya ubora kwa kuwa Serikali inatumia fedha nyingi katika kugharamia miradi hiyo.
- “Serikali inatoa fedha kwa ajili ya miradi ya maji alafu mnazitumia kujengea majumba na kununua magari, safari hii mtazitapika tunataka miradi itekelezwe kwa kuzingatia viwango.”
- Waziri huyo aliahidi kufuatilia kwa kina ujenzi wa miradi yote ya maji nchini ili kuhakikisha kama inalingana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa katika miradi hiyo.
Ad