- Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameungana na Waumini wa Kanisa Katoliki hapa nchini kuadhimisha Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara.
- Misa Takatifu ya maadhimisho ya Jubilei hiyo ambayo imefanyika Bagamoyo Mkoani Pwani ambako Ukristo uliingia mwaka 1868 imeongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Nairobi nchini Kenya Mwadhama John Kardinali Njue.
- Misa hiyo imehudhuriwa na Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa, Spika Mstaafu Anne Makinda, Maaskofu wa Majimbo yote ya Kanisa Katoliki hapa nchini na nchi jirani, Mapadre, Watawa na waumini wa Kanisa hilo kutoka majimbo yote hapa nchini.
- Akizungumza katika Misa hiyo, Mhe. Rais Magufuli amelipongeza Kanisa Katoliki kwa mchango lililoutoa kuwahudumia Watanzania kiroho na kutoa huduma za kijamii tangu miaka 150 iliyopita na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa katika kudumisha amani na upendo na kuwaletea wananchi maendeleo.
- Rais Magufuli amewashukuru Maaskofu, Mapadre, Watawa na viongozi wote wa Kanisa Katoliki kwa namna wanavyoshirikiana na Serikali na Madhehebu mengine ya dini katika kuleta maendeleo na kuimarisha ustawi wa jamii bila kubagua na amewaomba waendelee kukemea vitendo viovu vikiwemo uvunjifu wa amani, rushwa, ufisadi na ubakaji.
- Aidha, Rais Magufuli amewashukuru wananchi wa Bagamoyo kwa kuupokea Ukristo ambao uwepo wake umeleta manufaa makubwa kwa Watanzania na ameahidi kuwa Serikali itashirikiana na viongozi wa Kanisa hilo kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
- Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Gervas Nyaisonga amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuungana na Kanisa Katoliki katika Jubilei hiyo, amempongeza kwa kazi nzuri ya kutimiza ahadi alizozitoa kwa Watanzania katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake na ameahidi kuwa Kanisa Katoliki litaendelea kuliombea Taifa na kushirikiana na Serikali.
Ad