SERIKALI KUINUA ZAO LA KAHAWA NCHINI

Serikali imeamua kuanzisha minada ya kahawa kwenye maeneo ya uzalishaji kuanzia msimu wa 2019/2020 ili kuinua zao hilo la kimkakati nchini.

Hayo yamesemwa Bungeni Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo,  Omary Mgumba wakati akijibu swali Mhe. Bernadeta Mushashu kuhusu mpango wa Serikali wa kuinua zao la kahawa Mkoani Kagera ikiwemo kupandisha bei ili kumnufaisha mkulima.

Ad

Mgumba amesema kuwa lengo la utaratibu huo ni kuharakisha malipo na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa minada na kuwashirikisha wakulima wengi zaidi katika mikoa inayozalisha kahawa ikiwemo Mkoa wa Kagera.

Aidha, amesema kuwa katika kuboresha mazingira ya biashara ya zao hilo, Serikali inadhibiti makato yasiyo ya tija kwa wakulima yanayokatwa kwenye Vyama Vikuu vya Ushirika na Vyama vya Msingi ili kubaki na makato yanayolenga kuendeleza zao la kahawa.

“Kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB), Serikali imewezesha vyama vya ushirika vya kahawa kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kufanikisha shughuli za ukusanyaji na uuzaji wa kahawa ya wakulima hivyo kumpunguzia mkulima mzigo wa riba uliokuwa unatozwa na mabenki ya kibiashara,” amefafanua Naibu Waziri Mgumba.

Hata hivyo,  Mgumba ameongeza kuwa, Serikali imefuta tozo na kupunguza viwango vya makato mbalimbali vilivyokuwa vinatozwa kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kupunguza tozo zilizokuwa zinatozwa katika biashara ya kahawa pamoja na kupunguza viwango vya makato mbalimbali vilivyokuwa vinakusanywa na mkulima.

“Serikali pia  imepunguza kiwango cha ushuru wa mazao unaotozwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka asilimia tanohadi asilimia tatuya bei ya kahawa shambani,” amesema Mgumba

(Picha na Idara ya Habari-MAELEZO)

Ad

Unaweza kuangalia pia

MINADA 6 YA KOROSHO MSIMU WA MWAKA 2019/2020 YAINGIZA BILIONI 406.3

Zao la korosho katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020 limeingiza zaidi ya Bilioni 406.3 …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *