WACHIMBAJI WADOGO WILAYANI MBOGWE KUPATA UMEME NDANI YA SIKU KUMI

  • Wachimbaji wadogo katika machimbo ya Nyakafuru yaliyo katika Kijiji cha Nyakafuru wilayani Mbogwe wameonesha kufurahishwa na ahadi ya Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ya kufikisha umeme katika machimbo hayo ndani ya siku kumi.
  • Ahadi hiyo aliitoa jana mara baada ya kufanya ziara ya kikazi wilayani Mbogwe mkoani Geita ambapo akiwa katika machimbo hayo, wachimbaji hao walilalamika kuhusu gharama kubwa wanazotumia katika kununua mafuta ya kuendesha mitambo mbalimbali ikiwemo ya kuchenjulia ya madini.
WAZIRI WA NISHATI
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa umeme katika Kijiji cha Kasosobe, Kitongoji cha Mkolani wilayani Mbogwe. Wa Tatu kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Martha Mkupasi na wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga.
  • Kwa nyakati tofauti walieleza kuwa, mchimbaji mmoja anaweza kutumia zaidi ya shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya mafuta ya kuendeshea mitambo suala ambalo linawafanya kutopata faida inayostahiki katika shughuli zao.
  • Kutokana na hilo, Dkt Kalemani alisema kuwa, “kutoka umeme unapoishia hadi hapa ni kilometa 1.5 tu, na hapa kuna wachimbaji wadogo zaidi ya Elfu Nne na mashine za kuchenjulia madini zaidi ya 200, hivyo nakuagiza Meneja wa TANESCO kuleta umeme hapa ndani ya siku Kumi na pia muwafungie transfoma itakayohudumia eneo hili,”.
WAZIRI WA NISHATI
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa Tatu kutoka kulia) akiwa katika machimbo ya Nyakafuru yaliyo katika Kijiji cha Nyakafuru wilayani Mbogwe ambapo aliwaahidi wachimbaji wadogo wa eneo hilo kupata umeme ndani ya siku Kumi.
  • Waziri wa Nishati pia alitembelea mitambo ya kisasa ya kuchenjulia madini tani 10 kwa saa ambayo ipo katika Kijiji cha Shenda wilayani Mbogwe ambayo nayo uendeshaji wake unatumia mafuta  badala ya umeme.
  • Baada ya kukagua mitambo hiyo, Dkt. Kalemani alimwagiza Meneja wa TANESCO wilayani Mbogwe kuhakikisha kuwa, ifikapo tarehe 25 mwezi huu awe ameshafikisha  umeme katika eneo hilo.
  • Akiwa wilayani Mbogwe, Dkt Kalemani pia alikagua kazi ya usambazaji umeme katika Kijiji cha Bulugala na kukuta nguzo zimesimikwa huku nyaya zikiwa bado hazijavutwa hivyo alimuagiza mkandarasi wa umeme (kampuni ya Whitecity Guangdong JV) kuwasha umeme katika Kijiji hicho kabla ya tarehe 5 mwezi ujao.
KLM-4
Wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nishati aliyokuwa akiitoa katika Kijiji cha Ryobaila wilayanu Bukombe ambacho kimepata huduma ya umeme.
  • Katika ziara yake wilayani Mbogwe pia aliwasha umeme katika Kijiji cha Kasosobe, Kitongoji cha Mkolani ambapo awali alielezwa kuwa umeme huo bado haujafika katika maeneo muhimu ya kijamii kama Shule na Nyumba za ibada pamoja na vitongoji vingine vya Kijiji hicho.
  • Dkt Kalemani alimuagiza mkandarasi wa umeme kufikisha umeme katika vitongoji vyote vya Kijiji hicho ikiwemo ikiwemo Shule, na Nyumba za Ibada ndani ya siku 14.
  • Vilevile Dkt.Kalemani alifanya ziara katika wilaya ya Bukombe mkoani Geita ambapo aliwasha rasmi umeme katika Kijiji cha Ryobaika, kilicho katika Kata ya Uyovu na kutoa wasaa kwa wananchi kulipia huduma ya umeme mapema na wataalam wa TANESCO pamoja na mkandarasi kutokataa malipo ya wananchi kwa kisingizio chochote kile.
Ad

Unaweza kuangalia pia

MADINI NA VIWANDA VYALETA MAGEUZI YA UCHUMI NCHINI

Mauzo ya bidhaa nje ya nchi zisizo kuwa za kawaida yameongezeka kwa asilimia 41.9 kwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *