- Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kutumia busara katika kazi hiyo ili iwaongoze kufanya maamuzi sahihi hususan uunganishaji umeme katika taasisi na miradi ya umma.

- Alitoa wito huo kwa nyakati tofauti jana, Februari 25 mwaka huu, akiwa katika ziara ya kazi wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi.
- Akizungumza ofisini kwa Mkuu wa Mkoa na baadaye katika vijiji vya Kihuwe, Muungano na Mapochero, ambavyo aliviwashia umeme rasmi; Naibu Waziri alisisitiza kuwa pamoja na kila mkandarasi kuwa na wigo wa eneo analopaswa kuunganisha umeme, lakini siyo busara kwake kuruka taasisi za umma na miradi muhimu kama vile ya maji, afya na mingineyo kwa sababu tu iko nje ya wigo.

- “Unafika eneo, unaona Zahanati ile pale, akina mama wanajifungua gizani; Shule ile pale, kuna hosteli, unaziachaje bila umeme sababu tu hazipo ndani ya wigo! Mkandarasi unapaswa kutumia busara, ikibidi tuandikie sisi Serikali, tuone namna gani gharama husika zitalipwa ili maeneo kama hayo yasikose umeme,” alisema.
- Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alisema kuwa serikali inaendelea kujivunia kugundulika kwa gesi katika mikoa ya kusini na kwamba watanzania wanapaswa kufahamu kwamba serikali imedhamiria kuitumia ipasavyo.

- Akifafanua, alisema gesi inapaswa itumike katika viwanda vya mbolea, majumbani na katika kuzalisha umeme. Hivyo, aliwataka wananchi kupuuza maneno yanayosemwa na baadhi ya watu kuwa serikali haitoi tena kipaumbele kwa gesi iliyogunduliwa mikoa ya kusini.
- Naibu Waziri alifafanua zaidi kuwa, ili kupata umeme mwingi, wenye bei nafuu na wa uhakika; ni lazima serikali ihakikishe inatumia vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme ikiwemo maji, upepo, jua, gesi, tungamotaka na vinginevyo.
- “Ndiyo maana tunaanzisha miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme ambayo inatumia vyanzo mbalimbali, siyo gesi peke yake. Ni muhimu mkalitambua hilo kwamba, kama nchi, hatuwezi kutumia gesi peke yake katika kuzalisha umeme, tukaacha vyanzo vingine. Inabidi tutumie vyanzo vyetu vyote tulivyojaaliwa na Mungu.”

- Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme maeneo mbalimbali ya nchi hususan vijijini, Naibu Waziri alisema kazi hiyo inaendelea kufanyika kwa ufanisi ambapo sasa serikali imewaelekeza wakandarasi wa miradi hiyo kuhakikisha wanawasha umeme katika vijiji vitatu kila wiki kwa kila mkandarasi.
- Hata hivyo, aliwataka wananchi kuwa na subirá kwani kazi ya kuunganisha umeme inatekelezwa hatua kwa hatua.
- Naibu Waziri anaendelea na ziara yake mkoani Lindi ambapo amefuatana na wataalamu mbalimbali kutoka wizarani, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Ad