BUNGE KUHARAKISHA UANZISHWAJI SHERIA BODI YA WANAJIOSAYANSI NCHINI

 • Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limesema litaharakisha Mchakato wa Uanzishwaji Sheria ya Bodi ya Usajili wa Wanajiosayansi nchini ikiwemo kuishauri Serikali na kueleza kuwa, ni fursa nzuri ya kusimamia rasilimali madini na itapunguza hasara kwa wadau.
 • Kauli hiyo iliyotolewa Januari 23, jijini Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, William Ngeleja kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo Andrew Chenge na kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula inafuatia maoni yaliyotolewa na Wajumbe wa Kamati hizo ambapo wameeleza kuwa suala hilo lilichelewa.
3-01
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Edwin Igenge akiwakilisha Mada mbele ya Kamati za Kudumu za Bunge za Nishati na Madini na Sheria Ndogo.
 • Wajumbe hao wamekutana katika Semina maalum iliyoandaliwa na Wizara ya Madini kwa kamati hizo kwa lengo la kupitia na kutoa maoni katika Andiko la Waraka wa Bodi ya Usajili wa Wanajiosayansi nchini.
 • Kufuatia hatua hiyo, Bunge limeipongeza Wizara ya Madini kwa kuanzisha wazo hilo na kueleza kuwa, kutokuwepo kwa bodi hiyo kulipelekea  kufilisika na hasara kwa baadhi ya wadau wa madini ambao walipatiwa taarifa zisizo  sahihi za tafiti huku baadhi wajiolojia  wasio waadilifu wakitoa taarifa hizo wakijua siyo sahihi na  kuwasababishia hasara wawekezaji hususan wazawa.
1-01
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Prof. Shukrani Manya, akizungumza mbele ya Waheshimiwa Wabunge wa Kamati za Kudumu za Bunge (Nishati na Madini na Sheria Ndogo).
 • Pia, Ngeleja ameitaka Wizara kuhakikisha inazingatia nafasi ya wachimbaji wadogo wakati wa uanzishwaji wa sheria hiyo na kueleza kuwa wanapaswa kupewa nafasi wakati Taratibu na Kanuni mbalimbali kuhusu Sheria hiyo zinapoandaliwa.
 • Vilevile, amesisitiza kuhusu Wizara kutafakari kwa weledi suala la vyanzo vya mapato  kwa ajili ya kujiendesha baada ya kuanzishwa bodi hiyo na kueleza kuwa, suala hilo linatakiwa kuangaliwa kwa umakini ili kutoibebesha  serikali mzigo wa kuwa chanzo pekee cha mapato.
4-01
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo William Ngereja akizungumza jambo katika Semina ya Waheshimiwa Wabunge wa Kamati za Kudumu za Bunge (Nishati na Madini na Sheria Ndogo).
 • Wakitoa maoni yao, Mbunge Catherine Ruge ametaka Bodi hiyo kutokuwa chanzo cha mikwamo katika utekelezaji wa majukumu ya wanatasnia bali kuwa chombo cha kuwawezesha kukua.
 •  Naye, Mbunge wa Simanjiro, James Olle Millya amesema ‘’pamoja na kuchelewa kuanzishwa bodi hii labda hatujatumia rasilimali zetu kama wengine, naamini uwepo wa bodi hii utatuweka kwenye nafasi nzuri’’. Aidha, Millya ameishauri serikali kuangalia namna itakavyosimamia kampuni za kigeni zitakazo kuja kuwekeza nchini.
2-01
Mjumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge za Nishati na Madini na Sheria Ndogo) James Olle Millya akizungumzaa jambo mbele ya semina hiyo.
 • Akifungua Semina hiyo, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema imelenga kuweka uelewa wa pamoja ili kuwawezesha wajumbe wa kamati hizo kutoa maoni kutokana na umuhimu wao katika uanzishwaji wa Sheria ya bodi hiyo.
 • Aidha, ameongeza kuwa, wataalam wa jilojia nchini wamekuwa hawana chombo kinachowaongoza, taratibu wala sheria suala ambalo lilipeleka baadhi kutoa taarifa za uongo kwa wadau, na hivyo kupelekea hasara kwa kutoa taarifa za tafiti za madini zisizo sahihi.
5-01
Baadhi ya Wabunge walioshiriki Semina ya Kamati za Kudumu za Bunge (Nishati na Madini na Sheria Ndogo) wakifutilia semina hiyo.
 • ‘’ Tumekuwa nyuma sana kuanzisha chombo hiki, wenzetu walianza zamani mfano Sheria ya Local Content ipo kwa minajili ya kulinda nchi na wananchi na bidhaa zao. Tumeona kuja na chombo hiki kutasaidia kulinda haki zao, fursa za kulindwa na kutambuliwa kisheria,’’ amesisitiza Naibu Waziri Nyongo.
 • Ameongeza kuwa, Uwepo wa bodi hiyo utasaidia kudhibiti tabia hizo ikiwemo kuweka taratibu, wataalam wataongeza tija katika rasilimali madini na kutakuwa na chombo maalum cha kuwalinda.
 • Akiwasilisha andiko hilo, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Madini, Edwin Igenge pamoja na mambo mengine ameeleza umuhimu wa kuanzishwa bodi hiyo, majukumu  na muundo wa bodi ya usajili ya Jiosayansi, uhusiano wa bodi  hiyo na vyombo vingine.
 • Ametoa uzoefu kwa nchi nyingine za Afrika na Ulaya ambazo tayari zina bodi kama hizo tofauti na Tanzania na kuzitaja nchi za Kenya bodi yake ilundwa miaka 27 iliyopita, Afrika Kusini miaka 17 na Kanada miaka 20 iliyopita.
7-01
Baadhi ya Wabunge walioshiriki Semina ya Kamati za Kudumu za Bunge (Nishati na Madini na Sheria Ndogo).
 • Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Cha Madini Dodoma (MRI), Prof. Hudson Nkotagu amewaeleza wajumbe wa kamati hizo kuwa ni wataalam wenye sifa tu ndiyo watakaofanya kazi hizo na kuongeza kuwa, wagunduzi watatambuliwa.
 • Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizoibuliwa, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Prof. Shukrani Manya amewaeleza wajumbe hao kuwa, bodi hiyo inalenga kuwadhibiti wataalam wasio waaminifu wanaotafuta fedha kupitia taaluma hiyo huku wakiacha hasara kwa wadau na kuongeza kuwa, itasaidia kuleta weledi na kuwasaidia wadau kutokupoteza fedha zao.
 • Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Prof. Justinian Ikingura akitoa ufafanuzi kuhusu suala la sampuli hoja iliyoibuliwa na wajumbe wengi ameeleza kuwa, masuala ya maabara na sampuli yana maadili , na taratibu zake, hivyo, bodi hiyo itaepusha madhara mengi ambayo yamesababishwa  na wataalam wasiokuwa waaminifu.
Ad

Unaweza kuangalia pia

WAZIRI MKUU AMPONGEZA BONDIA SALIM MTANGO ALIYESHINDA MKANDA WA DUNIA WA UBO

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *