SERIKALI YAANZA RASMI BIASHARA YA KUUZA MAFUTA NCHINI

Na Zuena Msuya, Mara

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua rasmi biashara ya kuuza na kusambaza mafuta nchini  kwa kufungua   kituo cha kwanza kuuza mafuta ya Petroli na Dizeli cha Serikali kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kupitia Kampuni yake Tanzu ya Mafuta ( TANCOIL).

Ad

Aidha Dkt. Kalemani alisema kuwa kuzinduliwa na kufunguliwa kwa biashara hiyo ni kutimiza azma na nia njema ya Serikali ya kuboresha shirika lake la TPDC,kuwapatia na kuwasogezea karibu wananchi wake huduma ya kupata mafuta yenye viwango vya ubora unaotakiwa, bei nafuu, na yatakayopatikana kwa wingi muda wote.

Muonekano wa Kituo cha kuuza mafuta ya Petroli na Dizeli cha serikali (TANOIL)kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC) kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANOIL, kilichofunguliwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani,  Juni 06, 2020  wilayani Musoma mkoani Mara.

Dkt. Kalemani alifanya Uzinduzi huo pamoja na kufungua kituo hicho wilayani Musoma, mkoani Mara  Juni 6, 2020, wakati wa ziara yake ya kikazi  katika Mkoa huo, akiwa ameambatana na  Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Wizara hiyo na Taasisi zilizochini yake.

Alisema baada ya kuanza rasmi kwa biashara hiyo, TPDC kupitia TANCOIL itashirikiana na Halmashauri zote nchini kuhakikisha inafanikisha azma ya Serikali ya kufungua na kuweka vituo vya kuuza na kusambaza mafuta katika kila halmashauri nchini pamoja na miundombinu ya kuhifadhi na kusafirisha mafuta.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akikata sili katika gari iliyobeba mafuta, ili kufungua koki kuruhusu mafuta kuingia katika matanki ya kuhifadhi mafuta ya kituo cha kuuza mafuta ya Petroli na Dizeli cha TANCOIL,alipozindua rasmi biashara ya mafuta katika kituo hicho kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania( TPDC) kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANCOIL, kilichofunguliwa na Waziri huyo , Juni 06, 2020  wilayani Musoma mkoani Mara.

“Tumeshaanza biashara ya kuwauzia wananchi wetu mafuta, sitegemei kusikia mafuta yanauzwa kwa bei aghali katika vituo vya serikali, TPDC na TANCOIL mnielewe vizuri hapa!  hii haipo na haitakuwepo, lengo letu sisi serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wapata bidhaa bora za mafuta kwa kiwango kinachotakiwa,  kwa bei nafuu na yatapatikana kwa wingi wakati wote na huduma hii inapatikani jirani na  maeneo yao!,”Alisema Dkt. Kalemani.

Dkt. Kalemani aliwaeleza watanzania kuwa TPDC na TANOIL watashiriki katika biashara ya uagizaji na usambazaji mafuta kama zinavyofanya kampuni zingine za mafuta nchini ili kuongeza ushindani na kutanua wigo wa kampuni za kizalendo kushiriki  katika biashara ya mafuta, ambayo kwa sasa inafanywa na  makampuni kutoka nje ya nchi tu.

Alisema kuwa serikali kupitia TPDC itajenga vituo 100 kwa kipindi cha miaka 5 ijayo, tayari baadhi ya Halmashauri zimeanza kutenga maeneo yatakayojengwa vituo hivyo: Aidha itahakikisha kuwa nusu ya mafuta yote yanayoingizwa nchini yanasimamiwa TPDC.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Mara wakati  akifungua rasmi biashara ya mafuta katika kituo cha kuuza mafuta ya Dizeli na Petroli cha serikali(TANOIL) kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania( TPDC) kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANOIL, Juni 06, 2020,  wilayani Musoma mkoani Mara.

“Watanzania tutembee kufua mbele na kujivunia vilivyo vya kwetu! Uzinduzi wa biashara hii ya mafuta hapa Musoma leo unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, ya Uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli, ni kutambua juhudi na mchango mkubwa wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kuimarisha sekta ya Umma ya kukuza uchumi, pia hatuna budi kutambua mchango wake wa kuanzisha TPDC mwaka 1969 pamoja na kiwanda cha kusafisha mafuta cha TIPER mwaka huohuo, ambapo TPDC ilimiliki kiwanda hicho kwa asilimia 50%, mwalimu aliona na kuwaza mbali sana, hii yote ni katika dhana ya kujitegemea kiuchumi,”. Alisisitiza Dkt. Kalemani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini, (TPDC), Dkt. James Mataragio alisema kuwa katika kutekeleza azma hiyo ya serikali, kuanzia mwaka huu wa fedha 2020/2021, TPDC imetenga fedha za kutosha kwa ajili ya mtaji wa kugharamia shughuli za uagizaji, usambazaji na usimamizi wa mauzo ya mafuta nchini kote.

Dkt. Matagio, alisema kwamba TANOIL imejipanga kuhakikisha kuwa, kunakua na usalama wa usambazaji mafuta nchini yaani (security of supply), kunapatikana takwimu sahihi za mafuta, bei na viwango stahiki vya ubora, pamoja na uelewa mzuri na mpana wa biashara ya mafuta nchini.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Mara wakati wa ufunguzi wa kituo cha kuuza mafuta ya Dizeli na Petroli cha serikali kitakachosimamiwa na  TPDC kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANOIL, Dkt. Kalemani alifungua kituo hicho, Juni 06 ,2020, wilayani Musoma mkoani Mara.

“Ninafuraha sana leo TPDC inaandika historia mpya na kubwa sana katika nchi yetu, tunaungana na wakazi wa Mkoa wa Mara, kwa niaba ya watanzania wote kuonyesha furaha yetu katika kuandika historia hii mpya ya kwamba shirika letu na maendeleo ya Mafuta, (TPDC) linarudi kwa kishindo katika biashara ya kuuza na kusambaza wa mafuta ya Petroli, Dizeli na bidhaa zake kwa maslahi yetu sote na taifa kwa ujumla”, Alisema Dkt. Mataragio.

Alieleza zaidi kuwa Mwaka 2000, Serikali ilifanya maamuzi ya kuendesha biashara ya mafuta nchini kwa mfumo wa soko huria, hivyo TPDC ikaunda kampuni tanzu ya COPEC kuweza kuingia katika mfumo huo na kushiriki katika soko la ushindani katika biashara hiyo.

TPDC ilinunua na kujenga vituo mbali mbali nchini vikiwemo Segera na Muheza Mkoani Tanga, Makuyuni na Makumira Mkoani Arusha, Singida, Geita, pamoja Mkoani Mara ambapo vilinunuliwa vituo viwili tu cha Musoma na Tarime, vituo vyote hivyo vinamilikiwa na TPDC kwa asilimia mia moja(100% ).

Naibu Waziri wa Nishati , Subira Mgalu akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Mara wakati wa ufunguzi wa kituo cha kuuza mafuta ya Dizeli na Petroli cha serikali kitakachosimamiwa na  TPDC kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANOIL, Dkt. Kalemani alifungua kituo hicho, Juni 06 ,2020, wilayani Musoma mkoani Mara.
 

Dkt. alisema kuwa TPDC ilishiriki katika biashara hiyo kupitia katika vituo hivyo,hata hivyo kukosekana kwa Sheria madhubuti ya Mafuta/Petroli, kulififisha ushiriki wa TPDC katika soko lenye ushindani mkubwa.

Aliweka wazi kuwa baada ya kufanyika kwa michakato na mapitio ya rejea , maboresho mbalimbali ya shirika hilo pamoja na mambo mengine, kumewezesha Uwepo wa Sheria madhubuti, pamoja na usimamizi wa kanuni mbalimbali, ambazo sasa unaiwezesha TPDC kuingia katika soko kwa ufanisi zaidi.

Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015 imeipa TPDC hadhi ya kuwa Shirika la Mafuta la Taifa (NOC) ili kujiendesha kibiashara, kupitia Sheria hiyo, TPDC imeimarisha kampuni zake Tanzu za GASCO na TANOIL. Awali, TANOIL ilikuwa COPEC. Kampuni ya GASCO inajishughulisha na biashara ya gesi na TANOIL inajishughulisha na biashara ya mafuta, ambayo ndiyo biashara tunayoizindua leo Kitaifa.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Benki ya NMB Tanzania yapongezwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan

kwakuwa Kinara katika utendaji wake, kutengeneza faida kubwa ya mfano wa kuigwa na mashirika na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *