UTEKELEZAJI KATIKA SEKTA YA ELIMU

Hotuba ya Rais Magufuli wakati wa kufunga Bunge la 11 mjini Dodoma June 16,2020 Eneo la Elimu

”Kwenye elimu, kama unavyofahamu, tulianza kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari ambapo mpaka mwezi Februari 2020 tulikuwa tumetumia shilingi trilioni 1.01 kugharamia.

Ad

Lakini, mbali na kutoa elimu bure, tumeongeza idadi ya shule za msingi kutoka 16,899 mwaka 2015 hadi 17,804 mwaka huu; na shule za sekondari kutoka 4,708 mwaka 2015 hadi shule 5,330 mwaka 2020. Vilevile, tumekarabati shule kongwe za sekondari 73 kati ya 89, tumejenga mabweni 253 na vyumba vya maabara ya 227. 

Aidha, tumetoa vifaa kwenye maabara zipatazo 2,956 na tumepunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa madawati, ambapo idadi yake imeongezeka kutoka madawati 3,024,311 mwaka 2015 hadi kufikia 8,095,207; sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 200.

Kwa upande wa Vyuo vya Ualimu, tumekarabati vyuo 18, tumejenga upya vyuo viwili (Murutunguru na Kabanga) na halikadhalika tumepeleka kompyuta 1,550 kwenye vyuo vyote 35 vya ualimu kwa lengo la kuimarisha ufundishaji wa masomo ya TEHAMA. Kuhusu ngazi nyingine za elimu, tumeongeza Vyuo vya Ufundi (VETA) kutoka 672 mwaka 2015 hadi 712 mwaka 2020; na pia tumekarabati na kuboresha vifaa na miundombinu ya kufundishia katika vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi (FDC).

Vilevile, tumejenga hosteli, kumbi za mihadhari, mabwalo ya chakula na maktaba kwenye vyuo vikuu.Tumeongeza pia bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 348.7 mwaka 2014/2015 hadi shilingi bilioni 450 mwaka huu wa Fedha 2019/2020.

Kutokana na hatua hizo, uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza umeongozeka maradufu kutoka wastani wa wanafunzi milioni 1 mwaka 2015 hadi kufikia milioni 1.6 hivi sasa.

Aidha, idadi ya wanafunzi wa kidato cha I – IV imeongezeka kutoka 1,648,359 mwaka 2015 hadi 2,185,037.  Idadi ya wanafunzi wa VETA imeongezeka kutoka 117,067 mwaka 2015 hadi 226,767 mwaka 2020; na idadi ya wanafunzi wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) imeongezeka kutoka 6,693 mwaka 2016/17 hadi 9,736 mwaka 2018/19.

Kwa upande wa vyuo vikuu, idadi ya wanafunzi wanaojiunga mwaka wa kwanza imeongezeka kutoka 65,064 mwaka 2015 hadi 87,813 mwaka 2020; na wenye kupata mikopo wameongezeka kutoka 98,300 mwaka 2014/2015 hadi 130,883 mwaka 2019/2020. Kwa taarifa hii Waheshimiwa Wabunge, naamini nitakuwa sijakosea nikisema, kazi kubwa imefanyika kwenye sekta ya elimu.” Rais Magufuli Bungeni mjini Dodoma

Ad

Unaweza kuangalia pia

Uzinduzi wa Jengo Jipya la Makao Makuu ya UCSAF Dodoma: Kuimarisha Mawasiliano Vijijini

25 Aprili 2024, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *