TANZANIA NA UFARANSA ZASAINI MKATABA WENYE THAMNANI YA TSH BILIONI 592

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Frederic Clavier wakisaini moja ya Mikataba ya Mkopo nafuu wa shilingi bilioni 592.57 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Nishati ya Umeme unaounganisha Tanzania na Zambia, Mradi wa UmemeVijijini (REA) katika mikoa ya Tanzania Bara na Mradi wa Maji safi na Usafi wa Mazingira katika miji inayozunguka Ziwa Victoria Jijini Mwanza. Anayeshuhudia katikati ni Mwakilishi mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (ADF) Bi. Stephanie Essombe, Jijini Dar es Salaam.

Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) zimetiliana saini mikataba mitatu ya mikopo yenye masharti nafuu yenye jumla ya Tsh. Bilioni 592 kwa ajili ya miradi ya usambazaji wa umeme Vijijini , mradi wa umeme wa kuunganisha Tanzania na Zambia  pamoja  na kukamilisha mradi wa Maji Safi na Maji Taka katika miji inayozunguka Ziwa Victoria .

Mikataba ya mikopo hiyo imesainiwa leo Jumatatu (Juni 29, 2020) Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James kwa upande wa Serikali, Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Frederic Clavier na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa, Bi. Stephanie Mouen Essombe.

Ad

Bw. James alisema kuwa Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini utagharimu Euro milioni 100 (Tsh. bilioni 257.64) na utasambazwa katika mikoa 16 ya Tanzania Bara na Mradi wa Umeme wa Kuunganisha Tanzania na Zambia.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Frederic Clavier, wakibadilishana Hati za moja ya Mikataba ya Mkopo nafuu wa shilingi bilioni 592.57 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Nishati ya Umeme unaounganisha nchi za Tanzania na Zambia, Mradi wa Umeme Vijijini (REA) katika mikoa ya Tanzania Bara na Mradi wa Maji safi na Usafi wa Mazingira katika miji inayozunguka Ziwa Victoria Jijini Mwanza. Anayeshuhudia katikati ni Mwakilishi mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (ADF) Bi. Stephanie Essombe, Jijini Dar es Salaam

Bw. James alisema miradi yote mitatu ambayo imesainiwa inawiana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025, ambayo inaongoza juhudi za kuleta maendeleo nchini hadi mwaka 2025 na kwa sasa inatekelezwa kupitia Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP II) 2016/17 – 2020/21.

Alisema malengo ya Dira ni kuinua, kuratibu na kuelekeza juhudi za Watanzania, fikra na rasilimali za Taifa kwenye sekta muhimu ambazo zitawezesha nchi kufikia maendeleo na kuhimili ushindani mkubwa wa kiuchumi.

Kwa upande wa mradi wa maji, Bw. James alisema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha upatikanaji wa Maji kutoka mita za ujazo 33,000 hadi kufikia mita za ujazo 108,000 kwa siku pamoja na kuwezesha Mji wa Morogoro kupata kiwango cha mahitaji ya maji safi kinachokadiriwa kuwa mita za ujazo 126,253 kwa siku, ifikapo mwaka 2035.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James na Mwakilishi mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (ADF) Bi. Stephanie Essombe, wakisaini Hati za moja ya Mikataba ya Mkopo nafuu wa shilingi bilioni 592.57 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Nishati ya Umeme unaounganisha nchi za Tanzania na Zambia, Mradi wa Umeme Vijijini (REA) katika mikoa ya Tanzania Bara na Mradi wa Maji safi na Usafi wa Mazingira katika miji inayozunguka Ziwa Victoria Jijini Mwanza. Anayeshuhudia katikati ni Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Frederic Clavier, Jijini Dar es Salaam

Bw. James alisema Tanzania imekuwa ikinufaika na ufadhili wa AFD hususan katika sekta za Nishati, Maji, Usafirishaji na Kilimo kupitia idadi ya miradi  mbalimbali inayoendelea na ile inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Alisema miradi 7 inayoendelea kutekelezwa katika sekta mbalimbali hapa nchini kupitia misaada na mikopo inayotolewa wa Shirika hilo inafikia takriban Euro milioni 154.5 sawa na Tsh. Bilioni 387.6.

“Miradi 6 yenye thamani ya Euro milioni 141.4 kupitia ufadhili wa AFD imekamilika na kuna miradi mingine 12 yenye thamani ya Euro milioni 1,021.7 ambayo tuko kwenye mazungumzo na AFD katika sekta ya Nishati, Maji, Kilimo Usafiri wa mwendokasi Jijini Dar es Salaam, miundombinu ya viwanja vya ndege na Usafi wa mazingira Jijini Dare salaam” alisema Bw. James.

Aliishukuru Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa ufadhili huo muhimu, ambao utachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi na kupunguza umaskini na kuahidi kuwa Serikali itafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha kwamba fedha zitakazotolewa zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Stephanie Mouen Essombe aliahidi kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha inafikia malengo yake katika kuboresha maisha ya wananchi hasa katika upatikanaji wa maji.

“Ushirikiano wa Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) ulioanza miaka 20 iliyopita umezidi kuimarika ambapo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita Shirika limewekeza kiasi cha Euro milioni 258 sawa na takriban Sh. bilioni za Tanzania 655” alisema Bi. Essombe.

Alisema mradi huo umelenga kupanua Bwawa la Mindu linalochangia upatikanaji wa maji yanayotumika katika Mji wa Morogoro kwa asilimia 70 pamoja na kuboresha mfumo wa huduma ya maji taka katika mji huo.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo alisema kuwa mkopo huo utatatua changamoto ya maji ambayo ilikuwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa Morogoro.

Alisema mkopo huu unafaida nyingi nchini ikiwemo kutoa ajira pamoja na kutoa fursa kwa viwanda vya ndani kwa sababu vifaa vitakavyotumika kutekeleza mradi huo wa kihistoria vitanunuliwa ndani ya nchi.

Alisema hivi sasa Serikali inatekeleza miradi ya maji 1,423, miradi 792 imekamilika na miradi 631 inaendelea na kwamba mradi huo wa maji wa Mji wa Morogoro utakuwa mkombozi mkubwa wa wananchi wa mji huo.

Alisema upatikanaji wa fedha hizo ambazo mjadala wa kupata mkopo umechukua zaidi ya miaka minne utawezesha kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji nchini ambapo hivi sasa kiwango cha upatikanaji wa maji vijijini kimefikia asilimia 85 ya lengo la asilimia 95 iliyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM huku katika miji kiwango kimefikia asilimia 70.1 kati ya lengo la asilimia 85 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2020

Ad

Unaweza kuangalia pia

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA WOMENLIFT HEALTH

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Maelezo kutoka kwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *