TUFANYE KAZI KWA USHIRIKIANO ILI KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI – DKT GRACE MAGEMBE

Na WAMJW- ARUSHA

Mkurugenzi wa tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Magembe ametoa wito kwa Watoa huduma za Afya wote nchini kufanya kazi kwa kushirikiana baina yao na viongozi wao ili kuboresha huduma za afya nchini.

Ad

Dkt. Grace, ametoa wito huo wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya, na kuongea na Watumishi juu ya njia za uboreshaji huduma za afya katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha – Mount Meru.

“Ninawaomba sana tufanye kazi kwa umoja na ushirikiano, migongano na misuguano haileti maana yoyote katika kuwahudumia Watanzania, kama kuna mwenzetu katoka nje ya mstari, tuambiane ukweli na tuonyane bila kuleta misuguano” alisema Dkt. Grace.

Mkurugenzi wa tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Magembe (wakwanza kushoto) akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa uhakiki ubora Wizara ya Afya Dkt. Eliakim Eliud na Daktari katika wodi ya wagonjwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Arusha – Mount Meru.

Aliendelea kusema kuwa, Serikali imeendelea kujenga vituo vya kutolea huduma za afya, na kuboresha vilivyo chakaa, hivyo ni wakati wa watoa huduma kushirikiana kwa karibu na kufanya kazi kwa juhudi na ubunifu ili kuleta matokeo chanya katika utoaji huduma.

Hata hivyo, Dkt. Grace amesisitiza agizo la Mganga Mkuu wa Serikali juu ya kuongeza jitihada katika mapambano ya kuendelea kupunguza vifo vya mama na mtoto katika vituo vya kutolea huduma za afya, ndani ya miezi sita.

“Licha ya kuendelea kufanya Juhudi kubwa katika kupunguza vifo vya mama na mtoto, bado tuna namba kubwa ya vifo hivyo, kama Serikali inaongeza vituo na kuboresha huduma, kwanini vifo bado vipo juu, na mara nyingi vifo vingi vinaweza kuzuilika” alisema Dkt. Grace.

Mbali na hayo, Dkt. Grace ametoa rai kwa viongozi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha – Mount Meru kuhakikisha wanajiongeza ili kuongeza ukusanyaji mapato, jambo litalosaidia katika kuboresha huduma kwa wagonjwa.

Pia, Dkt. Grace ameagiza uongozi wa hospitali kuweka mpango mkakati mzuri wa matengenezo ya vifaa na kuhakikisha vipimo vyote vinafanyiwa uhakiki wa ubora na majibu yote yakaguliwe na yasainiwe na aliyepima na kuthibitishwa kabla ya kurudi kwa mgonjwa, katika ngazi zote ikiwemo maabara na mionzi.

Aliendelea kusema kuwa, kila muuguzi ni lazima awe na mpango wa huduma ya mgonjwa wake (nursing care plan), ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma kwa mgonjwa anaemhudumia.

Nae Mkurugenzi wa uhakika ubora wa huduma Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Eliakim Eliud ametoa rai kwa viongozi kushughulikia malalamiko ya wagonjwa kwa haraka, huku akiagiza namba za viongozi zibandikwe maeneo yanayoonekana na ziandikwe kwa kuonekana.

Aidha, aliwataka watoa huduma kutoa majibu kwa wagonjwa haraka pindi wanapowahudumia ili kufahamu wanasumbuliwa na shida gani, kuliko kuwapa dawa bila kuwapa mrejesho wa magonjwa yanayomsumbua.

Mbali na hayo, Dkt. Eliakim amewataka Watumishi wote katika maeneo ya kutolea huduma za afya kuboresha maadili, ikiwemo matumizi mazuri ya lugha kwa wanaokuja kupata huduma, kuanzia wanapoingia getini mpaka wanapomaliza kupata huduma, ili kupunguza malalamiko yasiyo na ulazima.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt. Alfello Sichalwe ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuboresha huduma katika Mkoa wa Arusha, huku akiahidi kuendelea kusimamia vizuri hali ya afya ikiwemo kupunguza vifo vya mama na mtoto katika Mkoa huo.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Askofu Dkt Maasa OleGabriel RAIS SAMIA ANATEKELEZA MAAGIZO YA MUNGU YA KUITUNZA BUSTANI YA EDENI

Askofu Dkt. Maasa OleGabriel Katibu Mkuu Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania na Askofu wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *