Na Zuena Msuya Lindi,
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC) itasambaza na kuunganisha bila malipo (bure) miundombinu ya usambazaji wa Gesi asilia kwa matumizi ya majumbani kwa wateja wa awali katika mikoa yote nchini itayofikiwa na huduma hiyo.
Dkt. Kaleamni alisema hayo wakati akizindua mradi wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia kwa matumizi ya majumbani katika Kijiji cha Mnazi Mmoja, mkoani Lindi, Mei 30, 2020 na kuwataka wakazi wa eneo hilo kuchangamkia fursa hiyo ili kujiletea maendeleo na kuondokana na uchafuzi wa mazingira, gharama kubwa za kununua mkaa na kuni pamoja na adha kutafuta kuni porini kwa ajili ya kupikia.
Aliweka wazi kuwa baada ya wateja hao kuunganishiwa miundombinu ya kusambaza gesi asilia katika nyumba zao,Taasisi kama vile Shule, Hospitali au sehemu za biashara kama vile Mahoteli, au Migahawa, mteja atawekewa mita ya kupimia kiasi cha gesi anayotumia itakayofanya kazi kama LUKU za umeme.
Alisema baada ya kufungiwa miundombinu hiyo ya kusambaza gesi asilia, mteja atatakiwa kununua uniti za gesi kulingana na mahitaji yake kama ilivyo katika umeme, na kuzitumia endapo zitaisha kabla ya kuongeza nyingine, mita itafunga hadi pale atakaponunua uniti zingine kuongezea, mfumo huo unaitwa malipo kabla ya kutumia( Pre- Paid System).
Aidha, Dkt. Kalemani alisema kwa familia ya watu sita(6) inakadiriwa kutumia kiasi cha gesi ya shilingi 30,000 tu, kwa mwezi kwa matumizi yote ya kupikia bila kubagua aina ya vyakula vinavyotumia muda mrefu jikoni kama vile Maharagwe ikilinganishwa na gunia la mkaa ama kuni.
“Watanzania wenzangu mnataka serikali iwape nini tena jamani,imegundua gesi asilia nchini kwetu inayotuzalishia umeme, sasa tunasambaziwa gesi hii majumbani ili tuitumie kupikia vyakula vyetu na hatulipii chochote wakati wa kuunganishwa kwa hawa wateja wa awali, zaidi tutalipia kile tunachotumia na ni gharama ndogo mno ukilinganisha na matumizi ya kuni na mkaa, hebu jitokezeni kwa wingi mfungiwe gesi katika majumba yenu”, Alisema Dkt. Kalemani.
Vilevile alieleza kuwa, serikali imeamua kufanya hivyo ili kuhamasisha matumizi ya gesi asilia iliyopatikana kwa wingi hapa nchini, pamoja na kupunguza ukataji wa miti hovyo kwa ajili ya kuni na kuchoma mkaa ili kusaidia juhudi za kutunza na kuhifadhi mazingira yetu.
Alisema mradi wa usambazaji wa gesi asilia ni endelevu, ambapo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 wateja wapya 2,000 wataunganishia gesi majumbani, 300 kati yao wanatoka Mkoa wa Lindi na vitongoji vyake.
“Wakina mama sasa mtaondokana na adha ya kutembea porini kutafuta kuni na kubeba mizigo ya kuni, pia matumizi ya gesi majumbani kutaimarisha na kudumisha ndoa na familia kwa kuwa hakutakuwa na sababu ya mtu kuchelewa kutoka kuokota kuni, au kuzamia porini akichoma mkaa, na hata mabinti zetu watakuwa salama zaidi”, alisisitiza Dkt. Kalemani.
Alitaja mikoa inayofuata sasa katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi asilia kuwa ni pamoja na Morogoro, Dodoma na Singida: Mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kwa kuwa na nyumba, mahoteli, viwanda na magari yanayotumia gesi asilia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC , Dkt. James Mtaragio aliwatoa hofu watumiaji wa gesi asilia majumbani kuwa usanifu na ujenzi wa miundombinu hiyo imezingatia hatua zote za usalama ili kuhakikisha matumizi ya gesi hiyo yanakuwa salama zaidi kwa mtumiaji na jamii kwa ujumla na hivyo kuwaomba wananchi kuondoa hofu katika matumizi ya gesi asilia kwa shughuli za kupikia.
“Usalama wa gesi hii unasababishwa na tabia yake kwani ni nyepesi kuliko hewa tunayovuta hivyo kama ikitokea imevuja basi hupotelea hewani mapema na haiwezi kulipuka wala kusababisha moto, vilevile usambazaji wa gesi hii ni salama zaidi kwa kuwa husambazwa katika mgandamizo mdogo kwa njia ya bomba tofauti na gesi nyinyine, ni imani yangu kuwa wananchi wengi mtatumia gesi hii kwakuwa ni salama zaidi na nigharama nafuu mno,” Alisema Dkt. Mataragio.
Akizungumzia gharama za matumizi ya gesi hiyo ikilinganishwa na mkaa pamoja na kuni,dkt. Mataragio Alisema kuwa kwa ulinganishi matumizi ya mkaa si chini ya shilingi 4,500 kwa wiki,wakati matumizi hayohayo kwa kutumia gesi ni shilingi 1000 tu.
Naye mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema kuwa Mkoa wa Lindi umeandika historia nyingine iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu ya ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia itakayokuwa ikitumika kwa kupikia majumbani, mahotelini kwenye taasisi za afya, elimu na matumizi mengineyo kama viwandani na kuendeshea magari.
Zambi aliishukuru serikali kupitia Wizara ya Nishati na TPDC kwa kutenga fedha zitakazowezesha utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa Lindi na baadae kote nchini aidha aliwashukuru wanalindi kwa ushirikiano waliouonyesha katika kipindi chote cha kutekeleza mradi huo na kuwaomba waendelee na moyo huo wa kizalendo