KATIBU MKUU WA MAWASILIANO AKUTANA NA BODI YA UCSAF

Na Prisca Ulomi, WUUM, Dodoma

Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainab Chaula amepokea changamoto kutoka kwa Bodi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ya huduma za mawasiliano ya redio ya uhakika kwenye maeneo mbali mbali nchini

Ad

Dkt. Chaula amepokea changamoto hizo  wakati wa ziara yake ya kujitambulisha kwa wajumbe wa Bodi ya UCSAF na kuzungumza nao kuhusu utekelezaji wa majukumu ya UCSAF ya kupeleka huduma za mawasiliano kwa wananchi waishio maeneo ya vijijini, yasiyo na mvuto wa kibiashara, mipakani na kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Justina Mashiba, akimkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainab Chaula (aliyeketi) alipowasili kwenye ofisi za Mfuko huo kujitambulisha na kuzungumza na bodi na Menejimenti ya Mfuko huo, Dodoma

Ameipongeza Bodi hiyo kwa kufikisha huduma za mawasiliano kwenye maeneo mbali mbali nchini ambapo hadi sasa asilimia 94 ya wananchi wanawasiliana. Aidha, ameiarifu Bodi kuwa wanafahamu changamoto walizonazo na wana majibu ya namna ya kutatua changamoto hizo na yeye yuko tayari kupokea ushauri wa kutatua changamoto walizonazo ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kupata huduma za mawasiliano ya simu na redio kwa kuwa redio inasikilizwa na wananchi walio wengi waishio vijijini bila kusahau usafirishaji wa vifurushi na vipeto kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa kutumia anwani za makazi na postikodi zilizopo nchi nzima pamoja na kuhakikisha kuwa huduma za tiba mtandao zinafika kwenye hospitali za ngazi ya kitaifa, rufaa na hata ngazi ya wilaya kwenye halmashauri 184 zilizopo nchini kote

Akizungumza na wajumbe wa Bodi hiyo, Dkt. Chaula amesema kuwa wote tunategemeana iwe unafanya kazi Serikalini au sekta binafsi kwa kuwa wote tunahudumia wananchi na wanatutegemea, hivyo kila mmoja atimize wajibu wake kwa kuwa tunachohitaji sisi ni mawasiliano

Mwenyekiti wa Bodi ya UCSAF, Dkt. Joseph Kilongola amemshukuru Dkt. Chaula kwa kuwatembelea na kujitambulisha kwao na kuwapa mwelekeo, kuonesha utayari wa kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za mawasiliano kuendana na matakwa ya Serikali ya kuhudumia wananchi wake

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainab Chaula (mwenye ushungi wa bluu) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara yake na ya Mfuko huo. Wa kwanza kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko huo, Dkt. Joseph Kilongola na wa kwanza kushoto kwake ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Justina Mshiba

Naye Mtendaji Mkuu wa UCSAF amempongeza Dkt. Chaula kwa kufika na kuzungumza na wajumbe wa Bodi na wa Menejimenti ya UCSAF kwa kuwa ameonesha njia, umoja na ushirikiano ambapo taasisi ilibidi ifike kujitambulisha kwake

Justina amesema kuwa, Menejimenti ya UCSAF iko tayari kushirikiana na Bodi na viongozi wa Wizarani ili kuhakikisha kuwa huduma za mawasiliano ya redio ya uhakika; usambazaji wa vifurushi na vipeto kupitia anwani za makazi na postikodi; na tiba mtandao zinaongezeka na zinafika kwenye hospitali mbali mbali nchini ili kurahisisha na kuharakisha utoaji wa huduma za tiba kwa ajili ya kuboresha afya ya wananchi waishio maeneo mbali mbali nchini

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wengine wa Bodi ya UCSAF, Gogfrey Simbeye, ambaye anawakilisha sekta binafsi kwenye Mfuko wa UCSAF, ameishukuru Serikali kupitia UCSAF kwa kutambua mchango wa sekta binafsi na kuishirikisha sekta hiyo katika kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi

Simbeye amesema kuwa Sekta ya Mawasiliano kupitia UCSAF imetekeleza vema sera ya Ushirikiano Baina ya Serikali na Sekta Binafsi (Public Private Partnership –PPP) kwa kutoa ruzuku kwa kampuni za simu kujenga minara ili kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi

Dkt. Chaula ameanza ziara hiyo ya kujitambulisha na kuzungumza na taasisi zake za Sekta ya Mawasiliano na wadau wake ili kuhakikisha kuwa watendaji wa Wizara, taasisi na wadau wanashirikiana kwa pamoja kwa kuzingatia kuwa Sekyta ya Mawasiliano ni Sekta nyeti na mtambuka ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa Sekta hiyo inaendelea kukua, kuchangia ukuaji wa uchumi na pato la taifa kwa maendeleo ya taifa letu

Ad

Unaweza kuangalia pia

PROF. KABUDI AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA MABALOZI WA UFARANSA, UTURUKI NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Pamalagamba Kabudi amekutana na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *