Na Zuena Msuya, Mtwara
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said amefanya ziara ya kutembelea na kukagua Miundombuni ya uchimbaji, uchakataji na usafirishaji wa gesi asilia katika Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Mhandisi Zena alifanya ziara hiyo mwishoni mwa juma kwa kukagua visima vya kuchimba gesi vilivyopo Mnazi Bay eneo la Msimbati pamoja na Kiwanda cha Kuchakata Gesi hiyo cha Madimba mkoani Mtwara na Kituo cha kupokea gesi na kufua Umeme cha Somanga Fungu mkoani Lindi, Mei 30- Juni 01,2020.
Mhandisi Zena alifanya ziara hiyo kwa lengo la kuona utendaji kazi wa mfumo mzima wa uchimbaji, uchakataji, usafirishaji wa gesi asilia na kufua umeme pamoja na matumizi mengine ya majumbani,mahotelini, viwandani na kwenye magari.
Baaada ya kukagua na kuona ufanyaji kazi wa mfumo huo, alilipongeza Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kwa kuendela kufanya kazi kwa weledi na uzalendo mkubwa.
“Huu ni mradi wetu sisi watanzania tunajivunia sana kuwa nao, hongereni sana TPDC mnafanya kazi nzuri sana na inaonekana, watanzania pia wanafahamu juu ya kazi yenu, uzalendo ndiyo kitu cha msingi kwa kila taifa ili liweze kuthamini vitu vyake vya ndani na kusonga mbele, wataalamu simameni imara kwa maslahi mapana ya taifa lenu, sisi serikali tunawapongeza sana” Alisema Mhandisi Zena.
Aliliagiza shirika hilo, kuendelea kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa wataalam wa mradi huo ili kuwajengea uwezo zaidi wa kitaaluma ili kukabiliana na ukuaji tekelolojia unaendelea kukuwa duniani kila siku.
Vilevile alitoa wito kwa wataalamu hao kuwa wasikubali kurubiniwa kwa namna yeyote ile, na kwa wale wakongwe na wenye uzoefu wa muda mrefu katika utekelezaji na usimamizi mradi huo,wasiwe wanyimi bali wawarithishe uzoefu na ujuzi zaidi vijana ambao ni wapya katika taaluma hiyo licha kuwa na elimu kubwa.
Pia aliwapongeza kwa kuendelea kutunza mazingira yanayozunguka mradi huyo uliodumu kwa miaka mitano sasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini, (TPDC) Dkt. James Mataragio alieleza kuwa mbali ya kuwepo kwa tishio la Virusi vya Corona nchini, uzalishaji wa gesi asilia haukuathirika badala yake uliendelea kuongeza kutoka futi za ujazo milioni siti hadi kufikia futi za ujazo milioni tisini.
“Corona haikuathiri kabisa uchimbaji na uzalishaji wa gesi asilia hapa nchini, tumeendelea kufanya kazi kwa kuchukuwa tahadhari, tukizingatia maelekezo ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto,Uzalishaji wa Gesi hadi kufikia Mwezi Aprili mwaka huu 2020 ilifikia futi za ujazo milioni 90, na umeme unaozalishwa sasa unatumia gesi hiyo pamoja na ule unaotokana na vyanzo vya maji”, Alisema Dkt. Mataragio.
Hii ni mara ya kwanza kwa Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Nishati kutembelea mradi huo wa gesi, baada ya kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo mapema mwaka huu.
Katibu Mkuu huyo pamoja na ujumbe wake, pia walitembelea kiwanda cha kutengeneza Malumalu pamoja na Mabox cha GodWill kilichopo wilayani Mkuranga mkoani Pwani kinachotumia gesi asilia inayochimbwa hapa nchini kufanya shughuli zake za uzalishaji.