NAIBU WAZIRI NDITIYE AELEKEZA SHIRIKA LA POSTA KUFANYA KAZI KIDIJITALI

  • Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amelielekeza Shirika la Posta Tanzania (TPC) kufanya kazi kidijitali kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
  • Mhandisi Nditiye amesisitiza kuwa wafanyakazi wa TPC wafanye kazi kidijitali zaidi kwa kuwa hivi sasa dunia inakwenda kidijitali na amewataka wahakikishe kuwa kila mahali nchini kuna ofisi za Shirika hilo na watoe huduma kwa kuzingatia matakwa ya wateja wao, wafanye kazi kwa bidii, uaminifu na ubunifu kwa kuwa kwa kufanya hivyo wanaongeza mapato ya Shirika na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa letu
1-01
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akisisitiza jambo kwa wajumbe wa mkutano wa 26 wa Baraza la wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania (hawapo pichani) wakati akifungua mkutano huo Dodoma. Wa pili kulia ni mwakilishi wa katibu Mkuu – Mawasiliano, kitolina Kippa na wa kwanza kushoto ni Posta Masta Mkuu wa Shirika hilo, Hassan Mwang’ombe
  • Amewapongeza wafanyakazi wa Shirika hilo na Menejimenti yake kwa kujiendesha wenyewe bila kutegemea ruzuku ya Serikali, kwa kutoa gawio na mchango kwa Serikali kwa kipindii cha miaka miwili mfululizo na kwa Shirika hilo kuondolewa kwenye orodha ya mashirika yaliyowekwa chini ya uangalizi wa Serikali kwa ajili ya kubinafsishwa
  • Katika hatua nyingine, Mhandisi Nditiye ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kukagua mabasi ya abiria yanayosafirisha vifurushi, vipeto na barua bila kuwa na leseni na kufuata utaratibu
3-01
Wajumbe wa mkutano wa 26 wa Baraza la wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania wakiimba wimbo maalumu wa wafanyakazi wakati wa ufunguzi wa Baraza hilo, Dodoma. Baraza hilo limefunguliwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani)
  • “Hadi sasa kuna mabasi ya abiria yanasafirisha barua, vifurishi na vipeto, TCRA wakague mabasi hayo asubuhi kama wanavyofanya LATRA na wakiona wamepakia bila leseni, mabasi hayo yachukuliwe hatua mara moja na waache kusafirisha bidhaa hizo mara moja,” amesisitiza Mhandisi Nditiye.
  • Amelitaka Shirika hilo kufanya biashara kwa kuwa wakipata wanarudisha gawio Serikalini na sio kila kitu kisafirishwe na mtu au taasisi binafsi kwa kuwa vitu vingine ni nyeti na hatuwezi kuruhusu mtu binafsi asafirishe damu za watu, vinginevyo mpaka asimamiwe na Serikali kupitia Shirika la Posta Tanzania
6-01
Mwakilishi wa Katibu Mkuu – Mawasiliano, Kitolina Kippa, akimkaribisha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) kufungua mkutano wa 26 wa Baraza la wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania lililofanyika Dodoma
  • Vile vile, ametoa rai kwa watanzania kutumia Shirika hilo kwa kuwa vitu havipotei na tuache kusafirisha vitu vya muhimu kama vyeti vya elimu ya juu kwingine kwa kuwa vikipotea mtoa huduma binafsi anakulipa shilingi 15,000/= tu ambayo haina thamani na cheti chako
  • Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Kitolina Kippa wakati akimkaribisha Mhandisi Nditiye alisema kuwa Shirika hilo linakutana kwenye mkutano huo ili kupanga mkakati wa utekelezaji kwa mwaka 2020/2021 ili kuboresha Shirika liweze kuchangia uchumi wa taifa letu
2-01
Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Hassan Mwang’ombe akifafanua jambo kwa wajumbe (hawapo pichani) wakati wa mkutano wa 26 wa Baraza la wafanyakazi wa Shirika hilo, Dodoma. Wa pili kushoto ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye aliyekuwa mgeni rasmi
  • Posta Masta Mkuu wa Shirika hilo, Hassan Mwang’ombe amemweleza Mhandisi Nditiye kuwa tayari Shirika linatoa huduma zake kimtandao ambapo malipo ya huduma yanafanyika kwa kutumia Mfumo wa Malipo wa Kielektroniki wa Serikali (Government electronic Payment Gateway – GePG)
  • Mwang’ombe ameongeza kuwa tayari Shirika lake limetayarisha huduma maalumu ya mtandaoni “android application” na sasa ipo kwenye majaribio ili kuweza kusogeza, kuharakisha na kurahisisha utoaji wa huduma na bidhaa za Shirika hilo kidijitali kwa wateja wake wa ndani na nje ya nchi kwa kuwa sasa dunia inakwenda kidijitali na Shirika lina ofisi zaidi ya 158 nchi nzima Tanzania Bara na Zanzibar.
4 -01
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akijadiliana jambo na Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Hassan Mwang’ombe (katikati) baada ya kufungua mkutano wa 26 wa Baraza la wafanyakazi wa Shirika hilo, Dodoma
  • Amefafanua kuwa katika mkutano huo, wajumbe watapatiwa semina kuhusu sheria za utumishi wa umma ili wajue haki na wajibu wao, watapatiwa mafunzo kuhusu mifumo mipya ya uendeshaji wa Shirika kidijitali ili kuwa na posta kiganjani pamoja na kupatiwa elimu kuhusu mfuko wa hifadhi ya jamii wa PSSSF.
  • Mkutano huo unahudhuriwa na wajumbe wa Shirika hilo kutoka Mikoa yote nchi nzima kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wapatao 90 ambao wanawakilisha wafanyakazi wa Shirika hilo jumla ya watumishi 775.Na Prisca Ulomi – WUUM, Dodoma
5 -01
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa tano kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa mkutano wa 26 wa Baraza la wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania lililofanyika Dodoma. Wa nne kulia ni Posta Masta Mkuu wa Shirika hilo, Hassan Mwang’ombe

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Ad

Unaweza kuangalia pia

NCHI ZA SADC ZATAKIWA KUTATHMINI UCHUMI WAKE BILA KUTEGEMEA MASHIRIKA YA KIMATAIFA PEKEE

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amesema kuwa nchi za Afrika hasa zilizopo …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *