SERIKALI YAPOKEA GAWIO LA SH. BILIONI 8.7 KUTOKA KWA MASHIRIKA NA TAASISI ZA UMMA

 • Serikali imepokea gawio na michango ya Sh. bilioni 8.7 kutoka kwa baadhi ya Mashirika, Kampuni na Taasisi za Umma, ikiwa zimebaki siku 15 kati ya siku 60 zilizotolewa na Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, za kuzitaka Taasisi, Kampuni na Mashirika hayo kutoa gawio kwa Serikali.
 • Gawio hilo limepokelewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango katika hafla iliyowakutanisha Wakuu wa Mashirika, Kampuni na Taasisi za Umma 13, jijini Dodoma.
S1-01
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango (Mb) akifafanua jambo wakati wa hafla ya kupokea gawio kutoka kwa Mashirika, Kampuni na Taasisi za Umma 13, jijini Dodoma, ambapo aliwahakikishia watanzania kuwa fedha hizo zitatumika kuboresha maisha ya wananchi wa hali ya chini.
 • Dkt. Mpango amewaagiza, Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi, Kampuni na Mashirika ya Umma ambao hawatatoa gawio ifikapo Januari, 23 saa sita usiku kujiondoa katika nafasi zao na wasisubiri barua.
 • Alisema kuwa ni vema kuhakikisha watu waliopewa dhamana katika Taasisi na Mashirika ya Umma wanatumia rasilimali zilizopo katika kuiwezesha Serikali kujitegemea kuliko kutegemea wafadhili ambao kwa sasa wanapeleka nguvu kubwa katika nchi zao.
S3-01
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango (Mb) (wapili kulia) akipokea gawio kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jaji mstaafu Damian Lubuva, katika hafla ya kupokea gawio kutoka kwa Mashirika, Kampuni na Taasisi za Umma 13, jijini Dodoma, kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb).
 • “Nawahakikishia kuwa fedha hizi zilizopokelewa katika Mfuko Mkuu wa Hazina zitatumika kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi masikini kwa kuwa Taasisi za umma zilianzishwa ili uwekezaji wake uwanufaishe wananchi na Taifa kwa ujumla”, alieleza Dkt. Mpango.
 • Dkt. Mpango amezishukuru Taasisi, Kampuni na Mashirika ya Umma kwa kutii agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa Novemba 24, 2019 lililozitaka taasisi hizo kutoa gawio ndani ya siku 60.
S6-01
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango (Mb) na Naibu wake, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) wakifurahia jambo na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jaji mstaafu Damian Lubuva, muda mfupi baada ya kupokea gawio kutoka kwa Mashirika, Kampuni na Taasisi za Umma 13, jijini Dodoma.
 • Alisema kuwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) liliingia ubia na Kampuni ya Star Media ya China kwa kipindi cha miaka kumi na kwa mara ya kwanza Kampuni hiyo imetoa gawio kwa Serikali la kiasi cha Sh. milioni 500, jambo ambalo linapaswa kusifiwa hasa kwa uongozi wa TBC ulio saidia kufanikisha jambo hilo.
 • Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, alisema kuwa ongezeko la maduhuli na michango kutoka kwenye Taasisi za umma kwa zaidi ya asilimia 552, sio jambo dogo na inatoa tafsiri kwa ulimwengu kuwa Tanzania sio masikini na sasa imeamua kusimamia rasilimali zake.
S2 -01
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akielezea kuwa ongezeko la maduhuli na michango kwa asilimia 552 kuwa ni ishara kuwa Tanzania imeamua kusimamia vema rasilimali zake, wakati wa kupokea gawio kutoka kwa Mashirika, Kampuni na Taasisi za Umma 13, jijini Dodoma.
 • Alisema kuwa ni muda wa kuwaambia wananchi kuwa ni wakati wa kufaidika na fedha zao za ndani ambazo Serikali yao iliwekeza kwa kuwa Rais ameamua kutumia rasilimali za Taifa kwa ajili ya maendeleo ya watanzania.
 • Naye Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka, alisema kuwa kati ya Taasisi 187 ambazo hazikutoa gawio na michango kabla ya agizo la Rais la Novemba 24 mwaka jana, tayari Taasisi 151 zimetoa gawio na michango hiyo hadi kufikia Januari 7, 2020.
 • Alisema kuwa mpaka sasa jumla ya Sh. bilioni 20.8 zimepokelewa katika Mfuko Mkuu wa Hazina, ambapo awamu ya kwanza katika kipindi cha kuanzia Novemba 25 hadi Disemba 11, zilipokelewa Sh. bilioni 12.1 na awamu ya pili kuanzia Disemba 12 mwaka jana hadi Januari 7 mwaka huu zimepokelewa Sh. bilioni 8.7.
S5-01
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango (Mb) (katikati), Naibu wake, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wapili kushoto), Manaibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Mary Maganga na Bw. Adolf Ndunguru (kushoto) pamoja na Msajili wa Hazina, Bw. Athuman Mbuttuka wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakuu wa Mashirika, Kampuni na Taasisi za Umma zilizotoa gawio la jumla ya Sh. Bilioni 8.7, jijini Dodoma
 • Bw. Mbuttuka, alisema kuwa taasisi ambazo bado hazijatoa gawio na michango ni 36, hivyo kuzitaka kuhakikisha zinatekeleza agizo la Rais la kutoa gawio hilo kwa kuwa ifikapo Januari, 23, 2020 saa sita usiku  Wenyeviti wa Bodi na Wakurugenzi wa Taasisi, Kampuni na Mashirika ya Umma wasiotekeleza hawatakiwi kuingia ofisini.
 • Miongoni mwa Taasisi zilizowasilisha gawio na michango ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Chuo cha Ushirika Moshi, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Star Media, Bodi ya Utalii, Shirika la Maendeleo la Taifa na Bodi ya Wataalamu wa Manunuzi na Ugavi (PSPTB).
 • Zaidi ya Sh. trillion 1.2 zimekusanywa kutoka katika Taasisi, Kampuni na Mashirika ya Umma 230 ikiwa ni gawio na michango mbalimbali kuanzia Novemba 24 mwaka jana hadi Januari 7, mwaka huu. Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Dodoma
Ad

Unaweza kuangalia pia

NCHI ZA SADC ZATAKIWA KUTATHMINI UCHUMI WAKE BILA KUTEGEMEA MASHIRIKA YA KIMATAIFA PEKEE

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amesema kuwa nchi za Afrika hasa zilizopo …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.