NIDHAMU YA MATUMIZI YA FEDHA YAONGEZEKA KWENYE HALMASHAURI NCHINI

Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota amesema uwepo wa nidhamu ya matumizi ya fedha kwenye Mamlaka za serikali za mitaa umechangia asilimia 95 ya Halmashauri kupata hati inayoridhisha kwenye ukaguzi.

Chikota ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC), alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akichangia hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kwa mwaka ulioishia juni 30, 2019.

Ad

Alisema taarifa ya CAG inaonyesha kuwa kati ya halmashauri 185 ziliokaguliwa,halmashauri 176 imepata hati inayoridhisha sawa na asilimia 95 na imetokana na nidhamu hiyo pamoja na usimamizi mzuri uliopo.

Alieleza kuwa hatua hiyo ni maboresho makubwa ikilinganishwa na kipindi cha nyuma ambapo Halmashauri nyingi zilikuwa zinapata hati yenye mashaka lakini kwa sasa ni halmashauri 9 sawa na asilimia 5 tu ndio zimepata hati yenye mashaka.

Hata hivyo, alisema pamoja na maboresho hayo bado kuna maeneo ya kufanyia kazi ikiwemo kwenye taratibu za manunuzi ambapo imeonyesha kuna ukiukwaji.

“Kwenye vitengo vya manunuzi ya serikali za mitaa kumeimarika kwa kiasi kikubwa lakini bado kuna dosari kama CAG alivyoonyesha kuwa amefanya ukaguzi wa kina katika halmashauri 74 na kukuta kuna manunuzi ya Sh.Bilioni 32.4 yamefanywa bila ya kushindanisha kama sheria ya manunuzi inavyotaka,”alisema.

Aliongeza “CAG pia amefanya ufuatiliaji wa kina kwenye mamlaka za serikali 47 na kukuta manunuzi yamefanyika bila ya kutumia tender board,na hii imechukua kama Sh bilioni  9.2,hapa afisa masuhuli angeweza kuzuia hoja hizi kwa kutumia tender board ambayo ipo kisheria kwenye mamlaka za serikali za mitaa.”

Kutokana na hilo, aliomba Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) kufuatilia udhaifu kama huo kwa halmashauri husika ambapo taarifa ya CAG ipo wazi na imezitaja halmashauri hizo.

 “Tujiulize kwa nini maafisa masuhuli wameamua kufanya hivi maana wanaturudisha nyuma, hoja kama hizi hazikuwa na sababu ya kuwepo kwenye taarifa kama hii,”alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Chikota alishauri Serikali kutoa ajira mpya kwa wahandishi katika halmashauri ili kuziba pengo lililoachwa na waliohamishiwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura).

Ad

Unaweza kuangalia pia

WAZIRI MWAKYEMBE AFUNGA MKUTANO WA MAKATIBU WAKUU WA NCHI WANANCHAMA WA SADC

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *