HUDUMA ZA AFYA ZABORESHWA BUNDA NA KUONDOA KERO KWA WANANCHI

Jonas Kamaleki, Bunda

Utoaji wa huduma za Afya umeboreshwa baada ya Serikali kutoa milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Bunda, mkoani Mara.

Ad

Baadhi ya wakazi wa Bunda wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwaboreshea na kuwasogezea huduma za afya hivyo kuwaondolea adha walizokuwa wakizipata kabla ya hatua hiyo ya Serikali.

Mkazi wa Kijiji cha Nyasula, Elizabeth Madimanya amesema kuwa Kituo kinatoa huduma nzuri na mandhari ya hospitali ni nzuri.

Naye Rehema Malila, mkazi wa Kijeti, Bunda ametoa pongezi kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuboresha huduma za afya.

“Zamani tulikuwa tunahangaika kupata huduma za afya mbali sana na kwetu hadi mtoto wangu alifia tumboni kwa kukosa huduma ya karibu, Kituo kinatoa huduma nzuri, watumishi ni wazuri, utadhani wote ni wachaMungu”, alisema Malila.

Kituo cha Afya Bunda kimekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa maeneo hayo ambao walikuwa wanafuata huduma za afya umbali mrefu zaidi ya kilomita 17.

Sehemu ya majengo ya kituo cha Afya Bunda mjini mkoani Mara baada ya kuboreshwa na kuanza kutoa huduma za upasuaji kwa wananchi wa mji huo na maeneo ya jirani.

Muuguzi Kiongozi wa Kituo hicho, Dorcas Makaya anasema Kituo cha Afya Bunda kinahudumia takriban akina mama watano kwa siku kwa ajili ya huduma za kujifungua. Anaelezea kuwa wanajitahidi kuwahudumia wananchi kwani dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa uhakika.

“Nawashukuru viongozi wa Halmashauri ya Bunda Mji kwa ushirikiano wanaotupatia kiasi kwamba tunatoa huduma bila wasiwasi, pia namshukuru Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa kutujengea Kituo hiki”, anaongeza Makaya.

Kituo hicho baada ya ujenzi wake kukamilika, kilianza kutoa huduma moja kwa moja baada ya Halmashauri ya Bunda kupata vifaa vya hospitali hiyo kutoka kwa wahisani toka nje.

“Hatukusubiri Serikali kutuletea vifaa ilibidi tujiongeze wenyewe kwa kuwasiliana na wahisani toka nje ili huduma zianze”, anaeleza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bunda Mji, Janeth Mayanja.

Kwa mujibu wa Mayanja Kituo hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Bunda Mjini na maeneo ya jirani kwa kusogeza huduma za afya karibu.

Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuboresha huduma za afya kwa kujenga zaidi ya vituo vya afya 362, hospitali za wilaya 67 ambazo hivi karibuni zimeagizwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Suleiman Jafo kuanza kutoa huduma mara moja baada ya kukamilika ujenzi wake.

Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa akisikika akisema kuwa Serikali yake imejipanga kuboresha huduma za afya kwa kuongeza bajeti ya Dawa na vifaa tiba kutoka Shilingi bilioni 31 hadi bilioni 270.

“Tumeajiri watumishi wa kada mbalimbali za 11,152, tumejenga nyumba za watumishi 306 na pia tumeboreshana kuimarisha huduma za kibingwa katika Hospitali yetu ya Taifa Muhimbili na Hospitali za Rufaa za Bugando, KCMC na Mbeya. Hivi sasa watu toka nchi jirani wanakuja nchini kupata matibabu ya magonjwa ya moyo, figo,kansa, mifupa ubongo na kadhalika”, anasema Rais Magufuli.

Hakika huduma za afya zimeboreshwa na kusogezwa karibu na wananchi hivyo kuwaongezea matumaini ya kuishi wakiwa na afya bora. Karibu wilaya zote hapa nchini licha ya kuwa na hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati vimejengwa na vingine kuboreshwa.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Mradi wa Magari ya Mwendo Kasi, Kuboresha Usafiri, Uchumi, na Mazingira Tanzania

Mradi wa magari ya mwendo kasi nchini Tanzania umekuwa na faida nyingi za kijamii, kiuchumi, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *