SERIKALI KUONGEZA IDADI YA NDEGE KUBEBA MINOFU YA SAMAKI

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akizungumza na Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, wakati wa mkutano wa pili wa kujadili namna ya kurahisisha usafirishaji wa minofu ya samaki kutokea Kiwanja cha Ndege cha Mwanza uliofanyika jijini Dodoma.

Serikali imewaahidi wafanyabiashara wa minofu ya samaki kuongeza idadi ya mashirika ya ndege yatakayosafirisha mzigo huo ili kuwafikia walaji kwa wakati.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, wakati wa kikao cha pili kilichowakutanisha Mawaziri wa Wizara tano zikiwemo Wizara za Mifugo na Uvuvi, Mambo ya Nje ya Nchi, Viwanda na Biashara, Fedha na Mipango na Kilimo.

Ad
Katibu Mkuu (Sekta ya Uchukuzi), Dkt. Leonard Chamuriho, akifafanua jambo kwa wataalam (hawapo pichani) wakati wa kikao cha pili cha kujadili namna ya kurahisisha usafirishaji wa minofu ya samaki kutokea Kiwanja cha Ndege cha Mwanza jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Mifugo na Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah.

“Mpaka sasa kuna mashirika zaidi ya mawili ambayo tunafanya mazungumzo nao ili kuleta ndege mkoani Mwanza, hivyo changamoto zilizojitokeza baada ya kuanza usafirishaji huo zinaendelea kushughulikiwa’, amesema Mhandisi Kamwelwe.

Waziri Mhandisi Kamwelwe, amesema baadhi ya changamoto ambazo zimeshashughulikiwa mpaka sasa ni pamoja na kuanza kwa ujenzi wa uzio na maboresho ya jengo la kutunzia mizigo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA), Bw. Gilliard Ngewe (kulia), akiteta na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama, wakati wa mkutano wa pili wa kujadili namna ya kurahisisha usafirishaji wa minofu ya samaki kutokea Kiwanja cha Ndege cha Mwanza uliofanyika jijini Dodoma.

Aidha, Waziri Mhandisi Kamwelwe amesema pamoja na jitihada hizo Wizara kupitia kamati iliyoundwa inaendelea kutafuta masoko ya samaki ili kufikia lengo la kusafirisha tani zaidi ya 100 kwa safari moja.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhanga Mpina, amesema pamoja na mzigo wa samaki na mabondo tayari uzalishaji wa bidhaa za nyama umeanza na wizara imejipanga kuhakikisha mzigo huo unasafirishwa nje ya nchi ili kuongeza pato la Taifa na wafanyabiashara wa bidhaa hiyo mkoani Mwanza.

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Emmanuel Bulayi, akifafanua jambo katika kikao cha cha pili cha kujadili namna ya kurahisisha usafirishaji wa minofu ya samaki kutokea Kiwanja cha Ndege cha Mwanza jijini Dodoma.

“Kwa Mkoa wa Mwanza peke yake uzalishaji wa nyama umeanza na matarajio ni kusafirisha zaidi ya tani hamsini kwa safari moja, kama Wizara tumejipanga vizuri kwenye jambo hili na huo ni mwanzo tu”, mesema Mpina.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,John Mongela ameishukuru Serikali kwa kushughulikia changamoto zilizojitokeza na kuahidi kuendelea kuhamasisha viwanda kuzalisha zaidi ili kuongeza pato na kuongeza ajira kwa wanaMwanza.

Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi (Uchukuzi), Mhandisi Aron Kisaka (kushoto), akizungumza na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama wakati walipokutana kujadili namna ya kurahisisha usafirishaji wa minofu ya samaki kutokea Kwanja cha Ndege cha Mwanza jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho amesema toka kuanza kwa usafirishaji huo mapema Aprili 22, mwaka huu, mpaka sasa tani zaidi ya 140 zimeshasafirishiwa ambapo mpango ni kusafirisha zaidi ya tani 100 kwa safari moja.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Mafanikio Na Umuhimu Wa Muungano Wa Tanzania: Sababu Za Kuunganisha Tanganyika Na Zanzibar

Kuunganisha Tanganyika na Zanzibar kulilenga kujenga umoja wa kitaifa na kuvunja mipaka ya kikanda na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *