UWEKEZAJI TUNAOUTAKA NI ULE WA KUWAJIBIKA KATIKA JAMII – WAZIRI KAIRUKI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akipokea maelezo kuhusu ufugaji wa ngamia katika shamba la Highland Estate kutoka kwa Mkurugenzi wa shamba hilo Bw. Pirmohamed Mulla alipotembelea moja ya uwekezaji wa kampuni hiyo ya ufugaji wa ng’ombe na ngamaia katika shamba hilo lililopo Kata ya Ubaruku Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ikiwa ni ziara yake ya kutembelea maeneo ya uwekezaji

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji Nchini Mhe. Angellah Kairuki amewataka wawekezaji wote nchini kujihusisha na jamii zinazowazunguka kwa kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuleta tija ya uwekezaji wao.

Ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kutembelea maeneo ya uwekezaji ili kukagua, kusikiliza na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika uwekezaji wao.

Ad
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akipokea maelezo kuhusu uvunaji wa kisasa wa mpunga kutumia mashine aina ya combine harvester zenye uwezo wa kuvuna tani 2.5 katika shamba la Estate kutoka kwa Mkurugenzi wa shamba hilo Bw. Pirmohamed Mulla alipotembelea shamba hilo lililopo Kata ya Ubaruku Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

Waziri Kairuki alitembelea Kampuni inayojishughulisha na kilimo cha Mpunga ya Highland Estate iliyopo katika Kata ya Ubaruku Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya Juni 26, 2020.

Akiwa katika ziara hiyo, Waziri Kairuki amewataka wawekezaji wote nchini kuwajibika katika jamii zinazowazunguka ili kuendelea kuwa na mchango chanya kwa jamii kwani kufanya hivyo kutaboresha mahusiano mazuri kati yao na jamii inayowazunguka.

“Tunawashuru kwa namna mnavyowajibika katika jamii, huo  ndiyo uwekezaji tunaoutaka, pamoja na nyie kupata faida ni vyema kuwajibika katika jamii inayowazunguka, jamii ambayo uwekezaji wako upo, tumeelezwa maeneo mengi ambayo mmetoa mchango wenu zikiwepo shule, kuchangia huduma za afya, mnavyojenga mabanio mapya, ujenzi wa kituo cha polisi na mengine mengi.”alisema Mhe. Kairuki

Afisa Mipango Wilaya ya Mbarali Bw. Emmanuel Kishimbo akisoma taarifa ya masuala ya uwekezaji katika Wilaya hiyo wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki alipotembelea katika Wilaya hiyo kukagua, kusikiliza na kutatua changamoto za wawekezaji katika sekta ya kilimo wilayani humo mkoani Mbeya.

Aidha alibainisha mikakati ya Serikali katika kuhakikisha inaboresha mazingira ya wawekezaji na wafanyabiashara nchini hivyo ni vyema kuzitambua na kuunga mkono jitihada hizo kwa vitendo na kuzikumbuka jamii zetu.

“Serikali kwa sasa inaendelea kuboresha mazingira bora ya biashara na uwekezaji, na kwa upande wa kilimo hii ni sekta ambayo tunaipa kipaumbele sana tukitambua kuwa ni sekta inayoajiri watu wengi lakini inamnyororo mrefu wa thamani na wanufaika ni wengi” alisema Waziri Kairuki

Kwa upande wake Meneja Msaidizi wa shamba hilo Bw. Sadiki Wigira alisema kuwa, sambamba na uzalishaji wa mpunga, kampuni inajishughulisha na kilimo cha Matunda, Mbogamboga, zao la korosho, ufugaji wa ng’ombe wa maziwa pamoja na ng’ombe wa nyama na vilevile wanamatarajio ya kuanzisha Kiwanda cha kusindika nyama na maziwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya Highland Estate Bw. Fahad Haroon wakati wa ziara yake katika shamba la mpunga linalomilikiwa na kampuni hiyo katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Bw. Aswege Kaminyoge amemshuruku Waziri Kairuki kwa kufanya ziara katika Wilaya hiyo na kutembelea kampuni ya Highland Estate kwani Kampuni hiyo pamoja na kampuni zingine zilizopo hapa zimekuwa zikitoa ushirikiano mzuri kwa Serikali kwa kulipa kodi zote za Halmashauri bila usumbufu na amewataka kuendelea kushirikiana ili kuboresha uchumi wa nchi yetu.

Mhe. Waziri Kairuki ameipongeza kampuni ya Highland Estate kwa uwekezaji walioufanya katikka eneo la Mbarali kwani uwekezaji huo umetoa ajira kwa wakulima zaidi ya 4,000 wa makundi mbalimbali pamoja na ajira za kudumu zaidi ya 310.

Vilevile zaidi ya wakulima 20,000 wamenufaika katika huduma mbalimbali zikiwemo huduma za ugani, mafunzo, vitendea kazi, pembejeo za kilimo, mbinu bora za kilimo pamoja na fursa za ardhi yao kwa wakulima wadogowadogo ambao hawamiliki ardhi.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS SAMIA ATEMBELEA RUKWA.. AANGAZIA AFYA, ELIMU, KILIMO NA MIUNDOMBINU KWA MIRADI YA MAENDELEO.

Katika ziara ya Rais Samia siku ya leo iliangazia kwenye sekta ya Afya, Elimu, Kilimo …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *