WAZIRI MKUU MAJALIWA – LENGO NI KUENDELEA KUJENGA MIRADI YA KIMKAKATI KWA MAENDELEO YA WATU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipoweka jiwe la msingi la upanuzi wa bandari ya Kasanga wilayani Kalambo, Julai 5, 2020. Wengine pichani kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino, Mhandisi Isack Kamwelwe na kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Josephat Kandege. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kudhibiti matumizi ya fedha za umma ili iweze kuendelea na ujenzi wa miradi ya kimkakati zikiwemo bandari kwa lengo la kuboresha maendeleo ya wananchi wake.
Pia, Waziri Mkuu amesema changamoto ya usafirishaji wa mizigo na abiria kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) itakuwa historia baada ya kuboreshwa na kujengwa kwa miundombinu ya bandari katika wa Ziwa Tanganyika ukiwemo upanuzi wa bandari ya Kasanga.
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumapili, Julai 05, 2020) alipozungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa Bandari ya Kasanga iliyoko wilaya ya Kalambo akiwa katika ziara  ya kikazi mkoani Rukwa. Mradi huo unagharimu zaidi ya sh. bilioni 4.7.
Alisema upanuzi wa bandari hiyo utawezesha mizigo inayotoka nchini kwenda Congo kufika kwa wakati kwa sababu itasafirishwa moja kwa moja bila kupitia katika nchi nyingine kama ilivyo sasa, ambapo madereva wanalazimika kupita kwenye Mataifa mengine na kutumia muda mrefu.
“Mradi huu ukikamilika utaongeza pato la mwananchi mmoja mmoja pamoja na Taifa kwa ujumla. Rais Dkt. Magufuli amedhamiria kuboresha maendeleo ya wananchi nchi nzima ikiwemo na wilaya hii ya Kalambo. Ujenzi wa miradi hii unatoa fursa za ajira kwa wananchi, hivyo zichangamkieni.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (kulia) ni Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly baada ya kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa bandari ya Kasanga wilayani Kalambo, Julai 5, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Vilevile, Waziri Mkuu alisema mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa bado yanaendelea nchini, hivyo mtu yeyote atakayebainika anajihusisha na masuala hayo atafutwe popote alipo akamatwe na achukuliwe hatua za kisheria kwa sababu rushwa ni adui wa haki.
Pia, Waziri Mkuu aliendelea kuwakumbusha watendaji ndani ya Serikali wahakikishe wananchi wanapofika katika maeneo yao ya kazi wawapokee, wawasikilize na kuwahudumia bila ya ubaguzi. “Hatuangalii sura wala kabila yeyote atakayekanyaga kwenye maeneo yenu ahudumiwe ipasavyo.”
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe alisema Tanzania na Congo zimeungana kwa Ziwa Tanganyika, usafiri wa barabara uliokuwa unatumika awali uliyalazimu maroli ya mizigo kupitia nchini nyingine na kuchelewa kufika.
Alisema kukamilika kwa upanuzi wa bandari hiyo pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwago cha lami kutoka Sumbawanga hadi Kasanga kutarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kwa kutumia bandari hiyo kuingia nchini Congo moja kwa moja bila kupita kwenye nchi juirani.
Waziri Kamwelwe alisema kuwa awali kulikuwa na changamoto ya barabara hali iliyosababisha meli kufika kwenye Bandari ya Kasanga na kulazimika kusibiri mizigo ambayo ilikuwa ikichelewa kufika kutokana na ubovu wa barabara na sasa tayari Serikali imeitatua kwa kuijenga kwa kiwango cha lami.
Awali, akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Kaimu Katibu Mkuu wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Uchukuzi, Mhandisi Thomas Ngulima alisema mradi huo umeanzishwa ili kuongeza ushindani na tija katika shughuli za kibandari kusini mwa Ziwa Tanganyika.
Alisema mradi huo unahusisha upanuzi mkubwa wa gati ilililopo sasa lenye urefu wa mita 20 lifikie mita 120, ambazo zitawezesha kuhudumia  meli mbili hadi sita kwa wakati. Kazi nyingine ni ujenzi wa miundombinu ya bandari ikiwemo jengo la kupumzikia abiria, mgahawa na nyumba za watumishi.
Mhandisi Ngulima alisema mradi huo unaojengwa na kampuni ya Inter-Consult Limited umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Septemba, 2020 na kwamba utafungua na kuboresha njia ya biashara ya mazao ya chakula katika nchi za DRC, Burudi na Zambia.
Aliongeza kuwa, ujenzi wa barabara ya kimkakati inayoanzia Manispaa ya Sumbawanga hadi Kasanga (km 107), pamoja na upanuzi wa bandari unaoendelea, utawezesha mtiririko wa shehena za saruji, makaa ya mawe, chokaa na sabuni kuongezeka hivyo kukuza uchumi wa wananchi na Taifa.

Ad
Ad

Unaweza kuangalia pia

Tanzania Yapiga Hatua Kubwa katika Miradi ya Maji, Zaidi ya Miradi 1,500 Yakamilika Vijijini na Mijini.

Tanzania imefanya maendeleo makubwa katika miradi ya maji, na hadi sasa, miradi mingi imekamilika ili …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *