PROF. SHEMDOE AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA WAZALISHAJI WA SARUJI NCHINI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe akizungumza na wamiliki wa viwanda vinavyozalisha saruji (pichani) kuhusu changamoto za bei ya saruji katika maeneo mbalimbali nchini, mkutano huo ulifanyika katika Eneo huru la Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje ya Nchi (EPZA), Jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu-MAELEZO.

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe, leo Julai 17, 2020 amekutana na wazalishaji wa Saruji nchini kujadili changamoto ya bei na upatikanaji wa bidhaa hiyo ambapo amewataka kuongeza uzalishaji katika viwanda vyao.

Ad

Akizungumza Katika kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa Eneo Huru la Uwekezaji kwa Mauzo Nje ya Nchi (EPZA) Ubungo External jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu  alisema kuwa sababu kubwa iliyofanya bidhaa ya saruji kupanda bei ni pamoja na kuwepo kwa mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha maeneo mbalimbali nchini.

“Katika Mkutano huu changamoto zilizoelezwa na wazalishaji wa viwanda vya saruji nchini ambapo imesababisha kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo ni pamoja na Mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha nchini nzima  katika kipindi cha mwezi Machi, Aprili na Mei ambapo iliathiri zaidi uzalishaji na usafirishaji wa Saruji”, Alisema Prof.Shemdoe

Aidha, Prof Shemdoe alisema kuwa changamoto ya mlipuko wa Ugonjwa wa Corona (COVID 19) ambapo iliathiri uzalishaji kutokana na kukosekana kwa vipuli vya mitambo inayotumika katika shughuli hiyo kwani huagizwa kutoka nje ya nchi.

Alibainisha kuwepo kwa upungufu wa bidhaa hiyo kutokana na Serikali kutekeleza miradi mikubwa inayoendelea nchini kama vile barabara za kisasa, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Ujenzi wa Bwawa kubwa la kuzalisha umeme (JNHPP) na ujenzi wa hospital mbalimbali hapa nchini, pia ujenzi wa mji wa Serikali na Ikulu mpya ya kisasa jijini Dodoma na ujenzi wa nyumba mpya za wakaazi jijini Dodoma.

Katika kikao hicho Prof. Shemdoe ametoa rai kwa  wazalishaji wa Saruji kuongeza uwekezaji na uzalishaji katika bidhaa hiyo ambapo kwa sasa ni muhimu kwa kuwa Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ambayo inahitaji saruji kwa wingi.

Aliongeza kuwa wazalishaji kwa sasa wanapaswa kuangalia fursa katika ujenzi wa miradi hiyo mikubwa na kujenga viwanda ili kuepusha gharama za usafirishaji wa saruji kufika katika maeneo ya ujenzi wa miradi, pia aliwashukuru kwa  kuitikia wito wa Serikali na kujadili hatma ya kuondoa kero ya kupanda kwa gharama na upatikanaji wa Saruji.

“Kikao hiki kimetoa mwongozo mzuri wa mwendelezo wa ushirikiano baina ya wawekezaji na Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali kwani kitendo cha wenye Viwanda kuridhia kwa pamoja kuongeza uzalishaji kufikia kiwango kilichokuwa awali pia kutokupandisha bei kitasaidia bei kushuka na Saruji kupatikana kwa wingi ndani ya muda mfup”, Alisema Prof.Shemdoe.

Nao Wawekezaji na Wazalishaji Saruji  nchini wamepongeza hatua hiyo iliyochukuliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwani imekuwa muhimili wa kuwaweka pamoja kuwasikiliza na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo na wamesema wapo tayari kushirikiana na Serikali katika kuboresha uchumi wa Nchi na Maisha ya Watanzania.

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *