WATENDAJI WA MIKOA WAHIMIZWA KUSIMAMIA USTAWI WA SEKTA YA FEDHA NCHINI

Na Farida Ramadhani, WFM, Morogoro

Serikali imewataka watendaji wa mikoa kuhakikisha wanasimamia na kuendeleza Sekta Ndogo ya Fedha nchini kwa kuhamasisha watoa huduma katika sekta hiyo wanasajiliwa na kukata leseni kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018.

Ad

Agizo hilo limetolewa na Kamishna wa Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja, wakati wa mafunzo ya Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha kwa watendaji wa mikoa ya Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Sngida na Iringa, yaliyofanyika katika hoteli ya Nashera mjini Morogoro.

Dkt. Mwamwaja alisema kuwa watendaji hao ni watu muhimu katika kuhakikisha Sekta ya Fedha nchini inastawi kwa lengo la kukuza uchumi na kuondoa umaskini nchini.

Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mameltha Mutagwaba, akihitimisha mafunzo ya Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha kwa watendaji wa mikoa ya Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa, yaliyofanyika mjini Morogoro.

“Mkitoka hapa mtakuwa kisima cha maarifa ambayo yatasaidia kutatua changamoto mbalimbali za sekta hii ambazo zimekuwa zikirudisha nyuma maendeleo ya wananchi. Nimatumaini yangu sasa changamoto zitakapo wasilishwa kwenu mtarudi kuangalia Sera, Sheria na Kanuni zinasemaje katika kutatua changamoto hizo”, alisisitiza Dkt. Mwamwaja.

Katika mafunzo hayo watoa mada walieleza miongozo na masharti mbalimbali yaliyoanishwa katika Sera, Sheria na Kanuni za Huduma ndogo za Fedha ya namna ya kuendesha biashara katika sekta hiyo zikiwemo taratibu za ukataji leseni na usajili.

Mwanasheria wa Serikali kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bi. Antelma Mtemahanji, ni miongoni mwa watoa mada hao ambaye alisema pamoja na Sheria hiyo watoa huduma za fedha nchini pia wanatakiwa kufuata Sheria zingine za nchi ikiwemo Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu.

Kamishina wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja (katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha watendaji wa mikoa ya Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa, iliyofanyika mjini Morogoro.

Alisema watoa huduma wa daraja la nne (vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha) wameruhusiwa kupokea akiba za wanachama wake, kukopesha wanachama wake pamoja na kukusanya michango mbalimbali ya uendeshaji wa kikundi hicho.

“Kikundi kinatakiwa kiwe na akaunti ya benki kwa ajili ya kuhifadhi fedha, jambo hili ni muhimu ili kuepuka upotevu wa fedha za wanachama kama ambavyo tumekuwa tukisikia na kuona kwenye vyombo vya habari mara kwa mara wanavikundi wakilalamikia kuibiwa fedha na watunza fedha wa vikundi hivyo, utasikia mama fulani alikua anatunza fedha mtoto wake kaiba kisanduku”, asisitiza

Bi. Mtemahanji alisema vikundi hiyo haviruhusiwi kufungua matawi au kuwa wakala wa benki, kupokea amana kutoka kwa wateja wasio wanachama na kukopesha watu nje ya vikundi vyao.

Aliwatoa hofu wanavikundi katika daraja hilo kwa mujibu wa Sheria kuwa vikundi vyao havitafungiwa bali vitaelelimishwa utaratibu wa kuvitambua na kuvisajili ili viweze kuendelezwa na kuchangia uchumi wa nchi.

Naye mtoa mada kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Deogratius Mnyamani alisema kuwa Sheria hiyo imeanisha misingi ya kumlinda mtumiaji wa huduma ndogo za fedha kwa kutoa miongozo mbalimbali ikiwemo utaratibu wa kukusanya madeni, uwazi katika utoaji wa mikopo  na ulipaji gawio kwa wanachama  wake.

Alisema sasa ni wakati wa kufuata Sheria na kuacha kasumba ya kudai kwa vitisho na kudhalilisha wakopaji kwa kuwa Sheria hiyo imetoa maelekezo ya kumtaka mkopeshaji kutoa elimu kwa kina kwa mkopaji namna ya kuulipa mkopo huo.

Bw. Mnyamani amewaonya wakopeshaji kutochukua kadi za kutolea fedha banki wakopaji kama dhamana ya mikopo wanayopewa kwa kuwa ni kinyume cha sharia na kwamba Sheria Mpya ya Huduma Ndogo ya Fedha imetoa miongozo ya dhamana za mikopo.

Kwa upande wake Mwanasheria kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika ambaye pia ni miongoni mwa watoa mada, Wakili Shanil Mayosa alisema kuwa Sheria hiyo kama Sheria zingine za nchi ina adhabu ambazo zitachukuliwa kwa watoa huduma watakaokiuka.

Alisema adhabu hiyo haijawekwa kwa ajili ya kuwatisha watoa huduma na wananchi kwa ujumla bali inalenga kuimarisha usimamizi, udhibiti na uendelezaji wa Sekta ya Fedha nchini.

Washiriki wa mafunzo hayo wameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwajali wananchi hususan wa hali ya chini ambao wamekuwa wakidhulumiwa na watu wasio waaminifu ambao wamekuwa wakitumia upenyo wa kutokuwepo kwa Sheria mahsusi inayosimamia Sekta Ndogo ya Fedha.

Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Bw. Robert George ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo ambaye aliishauri Serikali kutoa mafunzo kama hayo mara kwa mara katika masuala mbalimbali kwa maendeleo ya nchi.  

Mafunzo hayo ni muendelezo wa Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha uliozinduliwa Desemba mwaka jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, ili kuwawezesha wananchi kufuata matakwa ya Sheria na kuinusuru sekta ndogo ya fedha ambayo ni miongoni mwa sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Nchi.

Ad

Unaweza kuangalia pia

“Tusikubali Kuwa Tarumbeta za Watu Wasio Tutakia Mema”

“Tusikubali kuwa tarumbeta za Watu wasio tutakia mema, Maadili Yetu Mazuri Ya Kitanzania Lazima Tuyatunze, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *