MADAKTARI BINGWA WA UPASUAJI WA MOYO WAFANYA UPASUAJI WA KUPANDIKIZA MISHIPA YA DAMU KUTOKA KWENYE MSHIPA WA DAMU WA KIFUANI

Na Mwandishi   Maalum – Dar es Salaam

Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo, mishipa ya damu na kifua wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa mara ya kwanza wamefanya upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kutoka kwenye mshipa wa damu wa kifuani na kupeleka kwenye mishipa ya damu ya miguuni (Axillobifemoral Bypass Graft  Surgery).

Ad

Upasuaji huo ni wa kwanza kufanyika hapa nchini ambapo mgonjwa alikuwa na tatizo la kupata maumivu makali maeneo ya miguuni, mapaja na sehemu ya kukalia kwa muda wa miezi nane baada ya uchunguzi ikagundulika mshipa wake mkubwa wa damu (Abdominal  Aorta)  umeziba kabisa na hivyo kushindwa kupeleka damu kwenye miguu  (Aortoilliac Occlusion Disease) damu ilikuwa inapelekwa  kupitia mishipa midogo (Collaterals).

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana jijini Dar es Salaam daktari bingwa wa upasuaji wa moyo, mishipa ya damu na kifua wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Joseph alisema walimpokea mgonjwa huyo wiki iliyopita kutoka Hospitali ya Mnazi mmoja iliyopo   Visiwani Zanzibar.

Wataalamu wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika picha ya pamoja na Mama Fatma Khamis mkazi wa Zanzibar ambaye alifanyiwa upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kutoka kwenye mshipa wa damu wa kifuani na kupeleka kwenye mishipa ya damu ya miguuni (Axillobifemoral Bypass Graft  Surgery). Upasuaji huo ni wa kwanza kufanyika hapa nchini.
Picha na JKCI

Dr. Alex alisema  upasuaji wa aina hiyo haujawahi kuufanya hivyo basi baada ya majadiliano ya jopo la madaktari bingwa na kushauriana na mgonjwa waliona waufanye kwani kulikuwa na uwezekano mkubwa kwa mgonjwa kupona na kutoka katika maumivu makali aliyokuwa nayo.

“Upasuaji tulioufanya ni wa kupandikiza mrija bandia wa damu na kuukwepesha eneo ambalo  limeziba. Tuliweka  mrija kama mshipa bandia wa damu kutoka kwenye mshipa wa damu wa kifua upande wa kushoto na kuupitisha pembeni ya kifua na tumbo mpaka kwenye mguu wa  kushoto na kisha  kuelekea mguu wa kulia”,.

“Baada ya kufanya upasuaji huo  hivi sasa miguu yote miwili inapata damu ambayo inatoka moja kwa moja kwenye mshipa wa damu wa kifuani  kwani tuliikwepesha  eneo la tumboni ambalo mshipa umeziba”, alisema Dkt. Alex.

Dkt. Alex alisema hii ni faraja kwao kwani hivi sasa huduma za matibabu ya magonjwa kama hayo pamoja na mengine ya matatizo ya kuziba kwa mishipa ya damu zinapatikana hapa nchini na hakuna haja ya kusafiri kwenda kutibiwa nje ya nchi  ambako gharama ni  kubwa  kati ya milioni 15 hadi 20  wakati hapa nchini huduma inapatikana kwa gharama naafuu.

Kwa upande wake Mama Fatma Khamis ambaye alifanyiwa upasuaji huo alisema kwa muda wa miezi nane iliyopita miguu ilikuwa inamuuma baadaye akapata kidonda ambacho hakikupona hata baada ya kwenda Hospitali. Baadaye akaenda kwa  daktari wa mifupa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo Zanzibar ambapo baada ya kufanyiwa  vipimo  akaambiwa anatatizo la damu kuganda na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete(JKCI)  iliyopo Dar es Salaam kwani hospitali hiyo haikuwa na uwezo wa kumtibu.

“Baada ya kufika JKCI nilifanyiwa vipimo na kuambiwa mshipa   mkubwa wa damu haupitishi damu katika miguu na  hivyo kutakiwa kufanyiwa upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu niliambiwa katika upasuaji huo naweza kupona au la na hivyo kupewa fomu za kusaini nikasaini.

“Baada ya kufanyiwa upasuaji niko  vizuri kama unavyoniona naweza kusimama na kutembea vizuri maumivu ya miguu yamepungua tofauti na nilivyokuwa  mwanzo”, alisema Mama Fatma.

Aliwashauri watanzania wenye matatizo kama hayo wasipate tabu na wasihangaike kwenda kutibiwa nje ya nchi kwani hapa nyumbani ambapo ni karibu huduma hiyo inapatikana.

“Ninaishukuru sana Serikali yangu ya  Mapinduzi ya Zanzibar kwa kunilipia gharama za matibabu haya na sasa hivi nimefanikiwa niko vizuri”, alishukuru Mama Fatma.

Ad

Unaweza kuangalia pia

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA WOMENLIFT HEALTH

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Maelezo kutoka kwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *