Na. WAMJW-Dodoma
Serikali imefanikiwa kutimiza dhamira ya kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji na uwiano wa kutosha katika utoaji huduma za afya pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya za uhakika na wakati.
Hayo yamesemwa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi wakati akifungua kikao kati ya Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais-TAMISEMI cha kujadili utoaji huduma bora za afya kwenye vituo vya afya, Hospitali za Halmashauri na Rufaa zilizojengwa na kukarabatiwa na serikali ya awamu ya tano.
“Sisi kama wataalam tunawajibu wa kuendeleza chachu ya maendeleo yaliyofikiwa na kuhakikisha vituo hivi vinafunguliwa kwa kuzingatia utaratibu unaotakiwa na kuendelea kutoa huduma vikiwa na vifaa vyote muhimu na wataalam wenye weledi na stadi katika kupambana na magonjwa na kupunguza vifo vinavyozuilika”.Amesema Prof. Makubi.
Prof. Makubi ameongeza kuwa mafanikio hayo yamepatikana kufuatia sekta ya afya kuchukua jukumu la kufanya ukarabati wa ujenzi katika vituo vya kutolea huduma za afya ambapo iliweka kipaumbele kwenye vituo vya afya vya msingi ili kuviwezesha kutoa huduma za dharura za uzazi na mtoto mchanga.
“Tumejenga hospitali mpya za wilaya 99, kutoka hospitali 70 za awamu ya kwanza zimekamilika na nyingi zimeanza kutoa huduma hata hivyo serikali imeongeza kujenga hospitali nyingine 29 na fedha zake zimetengwa tayari”. Ameongeza Prof. Makubi.
Awali akiongea kwa niaba ya Naibu katibu Mkuu wa Afya TAMISEMI, Mkurugenzi wa huduma za Afya, Lishe na ustawi wa jamii Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa kikao hicho kina lengo la kuwa na muelekeo mzuri wa sekta ya afya hivyo ushirikiano wa pamoja kati ya Wizara hizo mbili ni muhimu katika kufanikisha na kusukuma mbele sekta hiyo nchini.
Naye Mkurugenzi wa huduma za kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi amesema kuwa vituo vya afya 570 vilivyojengwa na kukarabatiwa na Serikali vimeweza kuboresha huduma za afya na kuzuia vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga huku vikiwa na uwezo wa kutoa huduma za dharura kama upasuaji.