Katika kuhakikisha taifa letu linajenga uchumi ulio imara na jamii inayoheshimu na kufuata misingi ya uwajibikaji na ubunifu, Serikali pamoja na mambo mengine imeendelea kuwekeza katika elimu ya juu.
Serikali imeendelea kuhakikisha Watanzania wote wenye sifa wanapata elimu ya juu kwa kupewa mikopo kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, iliyoanzishwa chini ya kifungu cha Sheria Na. 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi Julai, 2005.
Bodi ya Mikopo pamoja na majukumu mengine, ina jukumu la kutoa mikopo au ruzuku kwa wanafunzi wenye sifa na wahitaji wa Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na mwombaji stahiki na mhitaji anaweza kuomba mkopo /ruzuku ili kugharamia sehemu ya gharama au gharama zote za masomo ya elimu ya juu.
Tangu kuingia madarakani kwa Rais Dkt. John Magufuli, Serikali ya Awamu ya Tano imeweza kuongeza bajeti ya maendeleo kutoka wastani wa asilimia 26 hadi asilimia 40 na hivyo kuweza kupanua wigo na kuboresha upatikanaji wa huduma za mbalimbali za jamii ikiwemo elimu ya Juu.
Katika kipindi cha miaka mitano cha Uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli Serikali imeongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka Tsh. bilioni 348.7 mwaka 2014/2015 hadi Tsh. bilioni 450 mwaka huu wa Fedha 2019/2020.
Kutokana na msukumo na juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali katika kuboresha elimu ya juu nchini, Serikali imeiwezesha na kuijengea uwezo Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kutekeleza vyema majukumu yake ya kisheria na kuongeza uwazi na ufanisi katika upangaji, utoaji na ukusanyaji wa mikopo.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi ya mwaka 2020/2021, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako anasema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu hadi kufikia machi 2020 imetoa mikopo yenye thamani ya Tsh. Bilioni 449.99 kwa wanafunzi 132,119 sawa na asilimia 99 ya fedha iliyoidhinishwa.
Prof. Ndalichako anasema katika ya hao, wanafunzi 49,799 ni wa mwaka wa kwanza na 82,320 wanaoendelea na masomo hatua inayolenga kutoa fursa na kupanua wigo kwa wanafunzi wenye sifa za uhitaji kujiunga na masomo katika vyuo na taasisi za elimu ya juu nchini.
Kwa mujibu wa Prof. Ndalichako anasema HESLB katika mwaka 2019/2020 pia imefanya ukaguzi kwa waajiri 2,406 nchi nzima na kutambua wanufaika wapya 14,731 wenye mikopo iliyoiva yenye thamani ya Shilingi Bilioni 100.7 ambapo kati yao wanufaika 13,969 (94%) wameanza kulipa.
‘Aidha, hadi kufikia Disemba, 2019 idadi ya wanufaika wanaorejesha mikopo ilikuwa imefikia 176,952 kati ya 184,166 waliotarajiwa sawa na asilimia 96 ya lengo’’ anasema Prof. Ndalichako.
Kwa mujibu wa Waziri Ndalichako anasema Bodi ya Mikopo imeendelea na ukusanyaji wa mikopo iliyoiva ambapo kiasi cha Tsh. Bilioni 144.3 kati ya Tsh. Bilioni 166.1 zilizolengwa katika kipindi cha mwezi Juni 2019 hadi Machi 2020 sawa na asilimia 86.9 zimekusanywa, ambapo lengo la makusanyo kwa mwaka lilikuwa ni kiasi cha Tsh. Bilioni 221.5.
Prof. Ndalichako anasema katika kusogeza huduma ya mikopo ya elimu ya juu karibu na wananchi pamoja na pamoja na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mikopo iliyoiva, HESLB imefungua ofisi ya Kanda katika Mkoa wa Mtwara na kufikisha jumla ya ofisi sita zilizopo katika Mikoa ya Dodoma, Mwanza, Arusha, Mtwara, Mbeya na Zanzibar.
Akifafanua Zaidi Prof. Ndalichako alisema Bodi ya Mikopo imeendelea kuboresha mifumo ya uendeshaji ili kuongeza uwazi na ufanisi wa utoaji huduma katika upangaji, utoaji na ukusanyaji wa mikopo iliyoiva, ambapo kwa sasa mifumo hiyo inamuwezesha mwanafunzi kupata taarifa za mkopo wake kupitia simu ya mkononi au mtandaoni na kuondoa usumbufu wa wanafunzi kufuatilia taarifa hizo kwenye ofisi za Bodi.
‘Bodi imebuni mfumo unaoviwezesha vyuo kuambatisha nyaraka muhimu kama vile matokeo ya mitihani kupitia mtandao badala ya kutuma nakala ngumu, vilevile uboreshaji wa mifumo umehusisha uunganishaji wa mifumo ya TEHAMA ya Bodi ya Mikopo na ya Tume ya Vyuo Vikuu ambapo taarifa za udahili za waombaji wa mikopo zinapatikana kwa urahisi na kwa wakati’’ alisema Prof. Ndalichako.
Ni dhahiri kuwa wigo wa utoaji elimu nchini unapanuka, hivyo ili kulinda ubora wa elimu ni wajibu wa mamlaka zote zinazohusika na usimamizi na udhibiti wa ubora wa elimu zitekeleze majukumu yao ipasavyo kwa kutoa miongozo na kufanya kaguzi za mara kwa mara.