HAMASISHENI WANANCHI KUJIUNGA NA CHF – WAZIRI MKUU MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Frank Chonya ahakikishe anawahamasisha wananchi wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kuwa na uhakika wa kupata matibabu.

Amesema kwa sasa Serikali iko katika mchakato wa kuwa na huduma ya bima ya afya ya Taifa, hivyo ni muhimu kwa wananchi wengi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ambao unawawezesha kupata bure huduma za afya kwa kipindi cha mwaka mzima.

Ad

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Desemba 30, 2020) wakati akizungumza na watumishi wa Hospitali ya wilaya ya Ruangwa alipotembelea hospitali hiyo akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Ruangwa, Lindi.

“Mkurugenzi hakikisheni fedha zote zinazokusanywa kupitia mfuko huu wa CHF zinaratibiwa vizuri na zinatumika kama ilivyokusudiwa. Mfuko wa Afya ya Jamii ni mkombozi katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi, ni lazima wahamasishwe kujiunga nao.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amemuagiza Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Dkt. Salvio Wikesi asimamie vizuri utoaji wa huduma kwa wagonjwa kwa sababu baadhi ya watumishi wanalalamikiwa kutoa lugha zisizofa kwa wananchi wanaokwenda kutibiwa hospitalini hapo.

“Watumishi hapa mnalalamikiwa lugha mnazozitoa kwa wagonjwa si nzuri, kila mmoja ajitafakari kuhusu utoaji wake wa huduma kwa wagonjwa. Badilikeni na muwe na lugha zinazowapa moyo wagonjwa. Taaluma ya utoaji huduma za afya inahitaji kujitoa.”

Waziri Mkuu amesema malengo ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 yanaelekeza kila kijiji kiwe na zahanati, hivyo amewaagiza madiwani kuweka kipaumbele cha ujenzi wa zahanati katika mipango yao ya maendeleo.

Baada ya kukamaliza kikao na watumishi wa hospitali, Waziri Mkuu amehutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Nachingwea wilayani Ruangwa ambapo amewahakikishia wananchi hao kwamba ataendelea kushirikiana nao kuboresha maendeleo ya wilaya hiyo. “Nitaendelea kuwa mtumishi wenu, tuendelee kushirikiana. Ruangwa kwa maendeleo inawezekana.”

Waziri Mkuu ametaja maeneo ya kipaumbele katika awamu hii kuwa ni uimarishwaji wa upatikanaji wa huduma za maji safi na salama, elimu na afya. “Suala la upatikanaji wa huduma ya maji ni endelevu, tutaendelea kuboresha miradi ya maji ili maeneo yote yapate maji ya uhakika.”

Amesema mbali na kuendelea kuboresha huduma hizo, pia atahakikisha uchumi wa wananchi wakiwemo vijana wajasiriamali unaimarishwa. “Katika kipindi cha miaka mitano hii kwa kutumia fedha za jimbo tutaimarisha shughuli za uchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo.”

Waziri Mkuu amewahamasisha wananchi wajikite katika shughuli zitakazowaingia kipato na wazisimamie vizuri ili ziweze kuwaletea tija. “Nitausimamia mfumo wa mikopo wa halmashauri ili uende kwa wananchi watakaotumia vizuri fedha hizo hasa wanyonge ambao ndio wahitaji.”

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *