Wizara ya Maji imekabidhi mradi wa maji wa Same –Mwanga –Korogwe (SMK) kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) baada ya kusitisha mikataba na kampuni za M .A Kharafi & Sons na Badr East African Enterprises Ltd.
Maamuzi ya Wizara ya Maji yanatokana na kusuasua kwa mradi huo kwa muda mrefu sasa huku wananchi katika maeneo ya wilaya za Mwanga ,Same na Korogwe mkoani Tanga wakiendelea kukabiliwa na changamoto ya huduma ya maji.
Katika mradi huo ambao chanzo chake ni Bwawa la Nyumba ya Mungu ,kampuni ya ukandarasi ya M.A Kharafi &Sons iliingia mkataba wa kujenga chanzo na mtambo wa kusafisha maji katika kijiji cha Njiapanda wilayani Mwanga pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kupeleka maji hadi katika tanki la Kisangara.
Katika hafla ya kukabidhi mradi huo kwa Dawasa Waziri wa Maji Jumaa Aweso alisema mkataba na kampuni hiyo ulisainiwa Nevemba 2014 ulitarajiwa kukamilika Julai 16,2017 na kwamba mkandarasi amekuwa akisuasua katika utekelkezaji .
“Hadi mkandarasi anasitishiwa mkataba Desemba 29,2020 uteklezaji wa kazi hii ilikuwa imefikia asilimia 64”alisema Aweso.
Waziri Aweso alisema mkataba mwingine ulikua ni usambazaji wa maji katika mji wa Mwanga na kujenga miundombinu ya kutoa maji Kisangara hadi kiverenge na kutoka Kiverenge hadi Mwanga mjini,kazi iliyokuwa ikifanywa na Mkandarasi BADR East African Enterprises Ltd.
“Kama alivyo mkandarasi wa kwanza huyu naye alisuasua katika utekelezaji wa mradi lakini pi aligushi nyaraka muhimu za kimkataba nakujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na hadi kufikia mwisho wa mwaka 2020 alikua amefikisha asilimia 60.
“Wizara ninayoiongoza imechukua maamuzi magumu ya kumsimamisha mkandarasi huyu Desemba 30,2020 “aliongeza Aweso Alisema mkataba namba nne unahusisha kazi za usambazaji maji katika mji wa Same na kujenga matenki manne na miundombinu ya kutoa maji Kiverenge hadi Same mjini kupitia mkandarasi BADR East African Enterprises Ltd ,mkataba ulionesha mkandarasi alipaswa kumaliza kazi Desemba 1,2019.
“Ni kwa sababu hii tuliona kuwa upo umuhimu wa Serikali yenyewe kupitia taasisi yake ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) yenye uzoefu wa utekelezaji na usimamizi wa miradi mikubwa ikamilishe kazi hii.” Alisema Aweso.
“Baadhi ya kazi kama Electro-mechanical works zitafanywa kupitia wakandarasi wenye uzoefu zaidi na kazi nyingine zitatekelezwa moja kwa moja na Dawasa” aliongeza Waziri Aweso. Aweso alimtaka Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja ahakikishe kuwa mradi unatekelezwa kwa wakati na kwa ubora kama ilivyo katika makabrasha ya usanifu .
Na Dixon Busagaga-Mwanga
Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cypriani Luhemeja alisema kazi ya ulazaji wa miundombinu ya maji katika maeneo hayo imeanza na kwamba wananchi katika wilaya ya Mwanga na Same wataanza kupata huduma ya maji ifikapo Novemba 30 mwaka huu.
“Kwa unyenyekevu kabisa mimi pamoja na timu yangu pamoja na Bodi inayoongozwa na Jenerali Davis Mwamnyange ,mkuu wa majeshi mstaafu,kazi hii tunaiweza na itakamilika tarehe 30 Novemba ,ninakuomba katika ratiba zako tarehe 19 Desemba tutakualika kuja kuzindua huu mradi”alisema Mhandisi Luhemeja .