RC MONGELLA AWATAKA WAFANYABIASHARA KULIPA KODI KWA WAKATI

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella amewataka wafanyabiashara kutumia fursa ya kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani hapa kulipa kodi kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo huku wafanyabiashara hao wakiishukuru Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa zoezi hilo ambalo linawaleta karibu walipakodi na wakusanya kodi.  

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni hiyo ambayo imeanza June 15 hadi 22 mwaka huu, Mkuu wa Mkoa huyo amesema kuwa, ni muhimu wafanyabiashara wote wakalipa kipaumbele suala la ulipaji kodi kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kugharamia huduma za jamii kwa manufaa ya kila Mtanzania.

Ad
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea jijini hapa.

“Kama mnavyojua umuhimu wa kodi na hasa katika kipindi hiki cha awamu ya tano hakuna Mtanzania ambaye hajashuhudia umuhimu wa kodi, tumeona barabara zikijengwa, ndege zikinunuliwa, ujenzi wa vituo vya afya, meli zikijengwa, ukarabati wa viwanja vya ndege ambavyo vyote vimesababishwa na uwezo wa serikali ambao umejengeka kwa mapato ya ndani,” alisema Mhe. Mongella.

Mhe. Mongella amesema kwamba, kutokana na faida hizo za kodi, ni muhimu wafanyabiashara wote wakatoa ushirikiano kwa maafisa hao wa TRA watakaopita katika maeneo ya biashara zao wakifanya zoezi hili la kutoa elimu ya kodi na kutumia fursa hiyo kupata uelewa na hatimaye waweze kulipa kodi ipasavyo na kwa wakati.

Amesema zoezi hilo limelenga kuwafikia wananchi na wafanyabiashara wa maeneo mbalimbali mkoani hapa yakiwemo Rwagasore, Pamba road, Buhongwa, Nyerere road, Misungwi, Mwaloni na Kisesa.

Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Patrick Massawe akimuelimisha Mfanyabiashara wa eneo la Karuta mkoani Mwanza kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi wakati wa Kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea jijini hapa
PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO

Sambamba na hayo amesema mambo yote yamefanikiwa kutokana na uadilifu na utendaji kazi wenye tija uliofanywa na serikali ya awamu ya tano katika kusimamia mapato ya ndani na kuyaelekeza katika kuimarisha uchumi wa nchi.

Frola Ayo ambaye ni mfanyabiashara wa mapambo na Charles Lyamuya mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi ni baadhi ya walipakodi waliopo Mtaa wa Lumumba na Karuta jijini hapa ambapo wameomba zoezi la utoaji elimu kwa mlipakodi liwe endelevu kwani linajenga urafiki baina yao na TRA na hivyo litaongeza uhiari wa kulipa kodi kwa wakati.

“Kutokana na elimu hii hakika tutalipa kodi ipasavyo kwa sababu inatuweka karibu na TRA suala ambalo linatuondolea hofu na pia tunaomba elimu hii iwe endelevu ili wafanyabiashara wengi waweze kujijenga zaidi na kuimarika katika biashara zao,” alisema Lyamuya.

Kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani Mwanza inafanyika pia katika Mkoa wa Morogoro na Mbeya na imelenga kuwaelimisha walipakodi juu ya mambo mbalimbali yanayohusu kodi ikiwa ni pamoja na kupokea maoni, kusikiliza kero na changamoto za walipakodi hao ili kuzitafutia ufumbuzi.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS SAMIA ATEMBELEA RUKWA.. AANGAZIA AFYA, ELIMU, KILIMO NA MIUNDOMBINU KWA MIRADI YA MAENDELEO.

Katika ziara ya Rais Samia siku ya leo iliangazia kwenye sekta ya Afya, Elimu, Kilimo …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *