TAARIFA KWA UMMA KUHUSU TANZANIA KUINGIA KWENYE KUNDI LA NCHI ZA KIPATO CHA KATI

Serikali ya Tanzania chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, imeandika historia baada Benki ya Dunia kuitangaza rasmi kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha kati kuanzia tarehe 1 Julai 2020.

Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, imeeleza kuwa Mhe. Rais, Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwa jitihada kubwa za kukuza uchumi wa nchi umeiwezesha Tanzania kuingia kwenye nchi za kipato cha kati miaka 5 kabla ya lengo lililoweka kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Ad
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu uamuzi wa Benki ya Dunia wa kuipandisha hadhi Tanzania kutoka kuwa nchi masikini hadi kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha kati kuanzia tarehe 1 Julai, 2020, Jijini Dodoma

Mheshimiwa Dkt. Mpango alifafanua kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 inatekelezwa kupitia mipango ya maendeleo ya miaka mitano mitano ambapo Mpango wa Kwanza wa Maendeleo ulitekelezwa kuanzia mwaka 2011/12 – 2015/16 ambao ulikuwa na dhima ya kufungulia fursa fiche za maendeleo na Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 una dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. 

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia Tanzania, ni miongoni mwa nchi tatu duniani zilizopanda na kuingia kwenye kundi la nchi za kipato cha kati kwa kundi la chini mwaka 2020. Nchi nyingine ni Benin na Nepal.

Katika Afrika kundi hili kwa sasa lina nchi 22, yaani Angola, Algeria, Kenya, Benin, Senegal, Lesotho, Tanzania, Cameroon, Tunisia, Comoros, Congo, Ivory Coast, Morocco Gibout, Egypt, Zambia, Eswatini, Nigeria, Zimbabwe, Ghana na Cape Verde.

Dkt. Mpango alisema kigezo muhimu kinachotumiwa na Benki hiyo  kuzitambua nchi zenye uchumi wa kati ni wastani wa Pato la Mwananchi (Per Capita GNI).

Nchi zenye uchumi wa kati huwa na wastani wa pato la taifa la kiwango cha kati ya dola za Marekani 1,036 (sh. 2,391, 088) hadi dola za Marekani 4,045 (sh. 9,335,860) kwa kundi la chini na dola za Marekani 4,046 hadi dola za Marekani 12,535 kundi la juu.  Vigezo vingine ni pamoja na kasi ya ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei na viwango vya kubadilishia fedha.

Alisema hatua hiyo iliyofikiwa ina manufaa mengi, yakiwemo kuongezeka kwa wigo wa upatikanaji wa fedha za mikopo ya kibiashara kwa ajili ya miradi ya maendeleo, kuvutia uwekezaji, kuwa na uhuru wa kupanga matumizi na kuondokana na kadhia ya utegemezi.  

Alimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, wadau mbalimbali wakiwemo wakulima, wavuvi, wafugaji, wafanyabiashara, wachimbaji wa madini, mabenki na wananchi wote kwa ujumla kwa mchango wao mkubwa ulioiwezesha nchi kufikia mafanikio haya

Aidha, aliwashukuru viongozi wenzake katika Wizara ya Fedha na Mipango na Benki Kuu ya Tanzania kwa jitihada kubwa za kusimamia uchumi kulikowezesha mafanikio haya makubwa.

“Pia ninaona fahari kwamba historia hii imeandikwa wakati nikiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Vilevile, Nimezungumza na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuhusu tukio hili na amefurahishwa sana kwa mafanikio haya makubwa na anawapongeza Watanzania wote kwa ushindi huu mkubwa” aliongeza Dkt. Mpango.

Ad

Unaweza kuangalia pia

WATAALAMU WA GST WAENDELEA NA UTAFITI WA MADINI PEMBA: KUKUZA MAENDELEO ENDELEVU KATIKA SEKTA YA MADINI

Katika utekelezaji wa Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya Wizara ya Madini Tanzania Bara na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.