MIFUMO YA FEDHA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI NI MUAROBAINI WA RUSHWA

Na. Peter Haule na Farida Ramadhani, WFM, Simiyu

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa, amewataka Watanzania kutambua umuhimu wa mifumo ya fedha iliyoanzishwa na Serikali kwa lengo la kupunguza vitendo vya rushwa na kuweka mazingira mazuri ya utawala bora.

Ad

Waziri Bashungwa amesema hayo alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.

Alisema kuwa rushwa itapungua endapo kiwango cha kukutana kati ya mtu na mtu kitapunguzwa hasa katika masuala yanayohusu fedha.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja (kulia), akiwaongoza Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa (katikati), Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Anthony Mtaka, kutembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.

“Mifumo ya fedha inayofanya kazi katika Serikali ya Awamu ya Tano ni ya Kielektroniki hivyo mtu anaweza kufanya malipo kwa njia ya simu ya mkononi katika ofisi yeyote ya Serikali bila kukutana na mtu, na hatua hii itapunguza mazingira ya ushawishi wa rushwa”, alieleza Mhe. Bashungwa.

Aidha, Mhe. Bashungwa, ameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuweka Sera nzuri za Fedha ambazo zimesaidia kuifikisha nchi katika uchumi wa kati miaka mitano kabla ya wakati uliokuwa unatarajiwa awali mwaka 2025.

Aliongeza kuwa Wizara yake itaishirikisha Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Taasisi ya Uhasibu Nchini (TIA) kutoa elimu  kwa wafanyabiashara wadogo na wenye viwanda kuhusu elimu ya biashara na utunzaji wa hesabu ili kuimarisha ujenzi wa uchumi wa viwanda.  

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa (kushoto) akipeana mkono na Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga, baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.

Akizungumzia Kilimo Mhe. Bashungwa ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2014-2019, Sh. trilioni 1.3 zilitumika kila mwaka  kuagiza nje yan chi chakula ikiwemo ngano na Mafuta ya kupikia, bidhaa zinazoweza kupatikana nchini endapo vijana wasomi wataangalia namna ya kuchochea mnyororo wa thamani wakati wa kuandaa Sera.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga, ameshauri suala la kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika vifungashio vya mazao ya ndani kama Pamba, Korosho na Kahawa liangaliwe upya ili kujenga ushindani dhidi ya mazao kutoka nje ambayo yamesemehewa kodi hiyo jambo litakalochochea ushindani na kulinda viwanda vya ndani.

Akieleza kuhusu biashara ya mazao ya kilimo wakati wa changamoto ya Covid 19, Mhe. Hasunga alisema kuwa baadhi ya nchi zimechukua hatua ya kufunga mipaka na kuzuia mizigo na wasafirishaji kuingia katika nchi mbalimbali zikiwemo nchi jirani.

“Sisi kama Wizara ya Kilimo pamoja na wadau wengine tumeathirika kwa kiwango kikubwa, tunakusudia kuwa na kikao cha pamoja katika maonesho haya ya Nanenane kati ya Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara Pamoja na taasisi zake ili tuzungumze namna tutakavyo kabiliana na changamoto ya ugonjwa huo”, alieleza Mhe. Hasunga.

Alisema kuwa kikao hicho kitaangalia namna bidhaa zinazoharibika haraka  kama maparachichi na mbogamboga zinaweza kusafirishwa kupitia Bandari za Tanga na Tanga badala ya kuzipeleka Mombasa.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja, aliwashukuru Mawaziri hao kwa kutembelea Banda la Wizara, Nyakabindi, Simiyu na kueleza kuwa Wizara inafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa sekta ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Viwanda vinachangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

Alisema kuwa Wizara imeondoa kodi zipatazo 114 zilizokuwa kero katika sekta hizo na hatua hiyo itaongeza tija ya uzalishaji na pia kuifanya nchi iendelee kuwa na usalama wa chakula na kuahidi kuzifanyiakazi changamoto zilizotolewa na Viongozi hao kwenye masuala ya kodi kwenye Sekta zao.

Ad

Unaweza kuangalia pia

TUIJENGE TANZANIA YETU

#Tanroads #SisiNdioWajenziWaTanzaniaYetu #SSH #CCM #KaziIendelee #Nchiyangukwanza #Sisinitanzania #Matokeochanya #MSLAC #SamiaSuluhuHassan #ChamaChaMapinduzi #PhilipMpango #NEMC #wizarayaafya

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *