NAIBU WAZIRI MABULA HARIDHISHWI NA KASI YA UPIMAJI NYANG’HWALE

Na Munir Shemweta, WANMM NYANG’HWALE

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameonesha kutoridhishwa na kasi ndogo ya upangaji na upimaji ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita.

Ad

Akiwa katika ziara yake ya kikazi kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi kwenye halmashauri hiyo jana, Dkt Mabula alisema kasi ndogo ya upangaji na upimaji maeneo umeifanya halmashauri ya Nyang’hwale kutoa idadi ndogo ya hati za ardhi na hivyo kuikosesha serikali mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Hati ya Ardhi Afisa wa Polisinye Halmashauri ya Mji wa Geita wakati wa zoezi la kugawa hati kwa wamiliki wa ardhi akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoa wa Geita jana.

“wilaya ya Nyang’hwale maeneo yake lazima yapangwe na kupimwa vizuri hatuwezi kulialia, hii wilaya mpya iwe wilaya ya mfano kuepuka ujenzi holela” alisema Naibu Waziri.

Kufuatia hali,  Naibu Waziri Mabula aliigiza ofisi ya ardhi mkoa wa Geita kwenda na timu ya wataalamu katika halmashauri hiyo wiki ijayo kusaidia kupanga na kupima maeneo sambamba na kupitia upya ramani za wilaya hiyo ili kuwa na dira itakayokuza Mji wa Nyang’hwale.

Dkt Mabula aliielezwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale Mariam Chaurembo kuwa idara ya ardhi kwenye halmashauri hiyo imekuwa na malalamiko mengi hasa kwenye kazi za upimaji maeneo aliyosema yanasababishwa na watumishi wa idara hiyo.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa halmashauri ya Mji wa Geita aliowakabidhi Hati za Ardhi akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoa wa Geita jana. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Alisema, pamoja na juhudi zake kuhakikisha maeneo mengi katika wilaya hiyo yanapangwa na kupimwa lakini watumishi wa idara ya ardhi  wamekuwa wasumbufu na wakati mwingine huondoka kituo cha kazi bila yeye kujua kwa kisingizo kuwa wako chini ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Naibu Waziri wa Ardhi alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang’hwale kuwawajibisha watumishi wote wa sekta ya ardhi watakaoonesha utovu wa nidhamu kwake na kusisitiza kuwa pamoja na Wizara yake kuwa na mamlaka ya nidhamu na ajira kwa watumishi wa sekta ya ardhi lakini hawaruhusiwi kuondoka kituo cha kazi bila mkurugenzi kujua.

Katika ziara yake ya kikazi mkoa wa Geita, Naibu Waziri Mabula aliitembelea pia halmashauri ya Mji wa Geita na kukagua Masijala ya Ardhi ambapo alionesha kutoridhishwa na utunzaji wa nyaraka za ardhi alioueleza kuwa unaweza kusababisha migogoro ya ardhi.

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *