Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Redio za kijamii zimeaswa kufanya kazi kwa ufanisi sambamba na kuzingatia maadili ya utangazaji hasa katika kipindi hiki cha kidigitali.
Akizungumza hivi karibuni jijini Dodoma, Afisa Habari kutoka Idara ya Habari- MAELEZO, Jonas Kamaleki wakati akifungua mafunzo maalumu yanayohusu masoko kwa kutumia mifumo ya kidigitali yalioandaliwa kwa mameneja masoko wa radio wanachama wa Mtandao wa Radio Jamii Tanzania (TADIO), alisema kuwa ni muhimu kwa redio hizo kutumia teknolojia hiyo ya mawasiliano ili kutoa habari kwa umma kwa mujibu wa sheria za taaluma hiyo.
“Mfumo wa kidigitali unasaidia kufikisha ujumbe na kupata wateja lakini pia unasaidia kuhakikisha habari zinawafikia wananchi kwa wakati, ni vyema kutumia ukuaji huu wa teknolojia kwa kusambaza habari ambazo zinachochea maendeleo sambamba na kutangaza utekelezaji wa miradi ya Serikali inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini”, alisema Bw. Kamaleki
Aidha, Bw. Kamaleki aliwataadharisha waandishi wa habari wa redio za kijamii kuwa licha ya teknolojia kusaidia kufikisha ujumbe kwa wakati, ina athari ambazo zinaweza kuleta madhara ikiwa haitatumiwa kwa manufaa ya nchi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa Vyombo vya Habari vyenye Maudhui ya Kijamii Nchini Tanzania (TADIO) Bw. Cosmas Lupoja alisema kuwa lengo la mafunzo hayo yanayofadhiliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamadunu la Umoja wa Mataifa (UNESCO) hapa nchini ni kuziwezesha radio Jamii kujitangaza na kutanua wigo wa masoko ili kuimarisha mapato yao.
Mafunzo hayo ambayo yamefadhiliwa na UNESCO ambapo ni mpango wa kuzijengea uwezo Radio Jamii kujitegemea, yanafanyika kwa siku 5 jijini Dodoma ikijumuisha redio jamii 34 chini ya Mwanvuli wa mtandao wa redio za jamii Tanzania Bara na Visiwani (TADIO).