Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kila Mtanzania anapaswa kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa wa amani na utulivu.
Amesema kuwa kiongozi wa nchi, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia watanzania kuwa uchaguzi utakuwa wa huru na haki.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Julai 31, 2020) wakati akishiriki swala na baraza la Eid el-Adh’haa iliyofanyika kitaifa jijini Dar es salaam.
“Naamini viongozi wa dini na kila mmoja tunaendelea kuliombea taifa hili ili uchaguzi wa mwaka huu umalizike salama, tujiepushe na lugha za uchochezi, tujiepushe na lugha za bezo, tujiepushe na lugha za kashfa, tuzungumze kile ambacho wananchi hawa utawatendea.”
Waziri Mkuu amesema kuwa kutokana na mfululizo wa matukio ya moto yaliyotokea katika taasisi za dini ya kislam ikiwamo Shule za Ilala Islamic na Kinondoni Muslim, Serikali kwa kushirikiana na vingozi wa dini hiyo wameanza uchunguzi ili kuibaini chanzo cha tatizo hilo.
“Hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria iwapo mtu yoyote atabainika kuhusika na matukio haya ya moto katika taasisi za dini ya kiislam, kama kulikuwa na dhamira ya mtu binafsi kuharibu miundombinu hii na kutia hasara kwa njama,hatuwezi kumvumilia na kama kutakuwa na makosa ya mifumo tutafuatilia na kufanya marekebisho makubwa.”
Amesema, Rais Dkt. John Magufuli pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan wanawatakia watanzania na waislam wote sikukuu njema ya Eid na amepokea salamu za pongezi zilizotolewa kwa Serikali na viongozi wa dini ya kiislamu namna Serikali inavyosimamia suala la amani nchini.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka waislam kujiepusha kutoa matamko ya mtu mmoja mmoja yanayoweza kuwavuruga waislam wote bali waendeleze mshikamano na mahusiano kwa waislam wote na taasisi nyingine
Naye, MuftiMkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally Mbwana amewataka watanzania kutambua kuwa uchaguzi mkuu ni wa watanzania wote, hivyo wanapaswa kuchagua viongozi wanaohitajika na ambao wataweza kukidhi haja za watanzania.
“Hakuna haja ya vurugu, ghasia wala kufanya fujo ya aina yoyote, tushikamane ili kuufanya uchaguzi vizuri, tumalize vizuri na kuijenga nchi yetu kwani sisi sote tunatakiwa tuijenge nchi.”