Katika jitihada za kuendeleza Diplomasia ya Uchumi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekubaliana na Jamhuri ya Namibia kuimarisha sekta za uvuvi na mifugo.
Makubaliano hayo yamefanyika leo jijini Dar es Salaam ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) amekubaliana na Naibu Waziri Mkuu Wa Jamhuri Ya Namibia ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Ndaitwah kuimarisha ushirikiano katika sekta ya Uvuvi pamoja na Sekta ya Mifugo.
“Tumekubalina kuimarisha ushirikiano katika enao la uvuvi wa bahari kuu lakini pia kuwahamasisha wadau wa sekta binafsi kutoka Tanzania na Namibia kuwekeza katika eneo hilo. Kwa upande wa mifugo na uuzaji wa nyama nchi za nje Namibia wamepiga hatua kubwa sana na sasa wanauza nyama Ulaya na Asia,” Amesema Prof. Kabudi
Aidha, Prof. Kabudi ameongeza kuwa wamekubaliana pia kuhamasisha sekta binafsi kutoka Namibia kuja kuwekeza katika machinjio na viwanda vya kusindika nyama hapa nchini (Tanzania) kwa ajili ya kuuza nyama hiyo nje ya Tanzania na kuendeleza sekta za uvuvi na mifugo.
Pamoja na mambo mengine, kikao cha leo kimepitia makubaliano ya miaka miwili iliyopita ambapo Tanzania na Namibia zimekubaliana kutumia fursa zilizopo kati yao kuendeleza sekta za uwekezaji, uvuvi, kilimo na mifugo kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu Wa Jamhuri Ya Namibia ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Ndaitwah amesema kuwa wamekubaliana kuimarisha sekta mbili ambazo ni Uvuvi na mifugo pamoja na kilimo kwa ujumla kwa kuzingatia mazingira bora ya uwekezaji na biashara ndani ya Umoja wa Afrika (AU).
“Kuna maeneo mbalimbali ambayo kwa pamoja tumekubaliana kuyaimarisha ikiwemo uvuvi, mifugo na kilimo kwa ujumla, kupitia kikao cha leo tunaamini kuwa wawekezaji kutoka Namibia watakuja kuwekeza Tanzania na vilevile wawekezaji kutoka Tanzania watawekeza Namibia,” Amesema
Ameeleza kuwa Namibia itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania katika kuhakikisha kuwa wanakuza uchumi wa nchi zetu zote mbili na Afrika kwa ujumla kwa kuzingatia misingi ya biashara na uwekezaji iliyopo ndani ya Umoja wa Afrika (AU).