Imeelezwa kuwa katika kipindi cha miaka mitano Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), umefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa Majengo ya Serikali 85 nchi nzima yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 142 ikiwamo miradi ya “Buni – Jenga”.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga, ameyasema hayo jjini Dodoma wakati akifungua mkutano wa mwaka wa 2020/2021 wa Baraza la Wafanyakazi wa wakala huo na kusisitiza kuwa hiyo ni hatua kubwa kitaasisi lakini hatua hiyo haijawaondoa moja kwa moja kwenye changamoto za kuchelewa kwa baadhi ya miradi ya ujenzi.
Mwakalinga ameutaka uongozi wa wakala kutazama kwa undani hatua gani walizofikia katika utekelezaji wa majukumu yao hususani namna wanavyoweza kushughulikia changamoto katika kila eneo la kiutendaji.
“Hakikisheni mnajitathimini kwa kina bado kuna changamoto za kuzifanyia kazi na Serikali yenu inawaamini katika utoaji ushauri na usimamizi wa miradi ya ujenzi na usimamizi wa miliki za Serikali”, amesema Katibu Mkuu huyo.
Aidha, ameupongeza Wakala kwa hatua nzuri waliyofikia katika miradi mbalimbali ya ujenzi ikiwamo ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota jijini Dar es Saalam ambapo hapo awali kulikuwa na malalamiko mengi.
Mwakalinga ameitaka TBA kuendelea kujali masuala ya wafanyakazi kutoka sekta binafsi kwa kuzingatia kuajiri watu wengi kwenye miradi ya ujenzi hususani walinzi, babalishe, mamalishe, watalaamu wa ujenzi, mafundi, vibarua na wanafunzi wa taaluma zote kutoka vyuo vikuu ili kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na kupunguza umaskini nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala huo, Arch. Daud Kondoro, amemueleza Mgeni rasmi kuwa katika mkutano huo wajumbe wa baraza la wafanyakazi watapewa elimu ya “haki za mtumishi mahali pa kazi na wajibu wa mtumishi kwa mwajiri” ili iweze kuwasadia kwenye utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.