Na Munir Shemweta, DAR ES SALAAM
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameanza kazi ya kuwatafuta wamiliki wa ardhi walioshindwa kuchukua hati zao kwenye ofisi za Ardhi za mikoa kwa kuwapigia simu wamiliki wa jiji la Dar es Salaam na kuwataka kuzifuata hati zao katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Desemba 29, 2020.
Jumla ya Hati 20,752 hazijachukuliwa katika ofisi za ardhi kwenye mikoa 26 ya Tanzania Bara na hivyo kufanya kuwepo mlundikano wa hati katika ofisi za Wasajili wa Hati Wasaidizi katika Ofisi za Ardhi za mikoa.
Miongoni mwa wamiliki wa ardhi waliopigiwa simu ni kutoka maeneo ya Salasala, Kibada na Mbezi Msakuzi Dar es Salaam ambapo baadhi yao walionesha kushangazwa na uamuzi wa Waziri Lukuvi kuwapigia simu na kuielezea hatua hiyo kama ishara ya kuonesha Wizara ya Ardhi imejipanga kuwahudumia wananchi.
Akitaja idadi ya Hati katika mikoa wakati wa zoezi la kuwapigia simu wamiliki hao leo tarehe 29 Desemba 2020 Lukuvi alisema mkoa wa Dar es Salaam ndiyo unaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya Hati 5,218 ambazo wahusika wameshindwa kuzichukua ukifuatiwa na mkoa wa Pwani wenye Hati 3,341 na Dodoma Hati 3,076.
Mikoa mingine na idadi ya Hati katika mabano ni Singida (201), Morogoro (1,345), Mtwara (470), Lindi (235), Ruvuma (118), Kilimanjaro (224), Manyara (143), Arusha (135), Tanga (711), Mbeya (266), Iringa (137), Njombe (45), Rukwa (23), Songwe (68), Kigoma (555), Tabora (626), Katavi (261), Mwanza (1,532), Geita (251), Simiyu (213), Kagera (382), Shinyanga (817) na Mara (559).
Lukuvi amewahimiza wananchi kujitokeza kuchukua hati kwenye ofisi za ardhi za mikoa na kusisitiza kuwa, hivi sasa wamiliki wamerahisishiwa uchukuaji hati katika ofisi za ardhi za mikoa tofauti na huko nyuma ambapo walilazimika kusafiri mpaka ofisi za kanda zilizohusisha zaidi ya mikoa miwili.
Alisema, mmiliki yoyote wa ardhi anayejua amelipia kodi pamoja na tozo zote ajue kwamba ni miongoni mwa watu ambao hati yake imekamilishwa na iko katika ofisi ya Msajili wa Hati.
“Tafadhali kama una hati na kiwanja kilichopimwa na umelipa kodi na tozo zote za kutayarishiwa hati nenda ofisi ya ardhi mkoa umtafute msajili wa hati ili uthibitishe na uchukue hati, tunataka zoezi hili liishe haraka kila mwenye hati afuate mwenyewe na kama kuna kodi anadaiwa alipe” alisema Lukuvi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwataka makamishna wote Wasaidizi wa Ardhi katika mikoa kuhakikisha wanafuatilia katika kila wilaya na kuangalia aliyemilikishwa kama hajachukua hati akachukue mwenyewe na isiwe zaidi ya siku 30 kuanzia tarehe 29 Desemba 2020.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka wamiliki wa ardhi wanaotaka kujenga kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu zote wakati wa kufanya ujenzi.
Lukuvi alisema, sheria inamtaka mmiliki wa ardhi anayetaka kufanya ujenzi kupata kibali kutoka halmashauri za miji, manispaa na majiji na kuongeza kuwa sheria hiyo inakataza kufanya ujenzi bila kibali kutoka mamlaka husika.
” Naelekeza watendaji wote wawe wa ardhi au mipango miji kuhakikisha sheria zinafuatwa kwa kudhibiti ujenzi holela na sheria inakataza kabisa kujenga bila kupata kibali kutoka katika mamlaka husika” alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, zoezi la urasimishaji linaloendelea sasa maeneo mbalimbali ni kwa majengo yaliyojengwa tu na kusisitiza kuwa zoezi la urasimishaji isiwe sehemu endelevu ya kuvunja sheria na kubainisha kuwa angetaka kuona maeneo yote ya miji hasa Dodoma yanajengwa kwa kupatiwa kibali.
Aliwataka wataalamu wote hasa waliopo halmashauri katika yale maeneo yaliyotangazwa kimji kwa mujibu wa sheria wananchi wake waelimishwe kujenga katika viwanja vilivyopangwa na kupimwa na wawe wamepatiwa vibali na mamlaka za halmashauri husika.
” hatua zichukuliwe kuzuia jambo hili tunataka miji endelevu ambayo wananchi wanaishi na kujenga kwa mujibu wa sheria” alisema Lukuvi