RAIS MUSEVENI AFANYA ZIARA YA SIKU MOJA HAPA NCHINI KWA KUMTEMBELEA RAIS MAGUFULI KIJIJINI KWAKE CHATO GEITA

 • Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni leo tarehe 13 Julai, 2019 amefanya Ziara Binafsi ya siku 1 hapa nchini kwa kumtembelea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli nyumbani kwake katika Kijiji cha Mlimani Wilaya ya Chato Mkoani wa Geita.
MM 2-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mgeni wake Rais wa Uganda Yoweri Museveni mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Chato mkoani Geita.
 • Mhe. Rais Museveni aliyetua katika uwanja wa ndege wa Chato akitokea nchini Angola amepokelewa na Mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli na kisha viongozi hao wakawasalimu wananchi wa Chato na viongozi mbalimbali waliokusanyika uwanjani hapo kwa ajili ya kumlaki.
MM 12-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimsindikiza mgeni wake Rais wa Uganda Yoweri Museveni wakati akiwapungia mkono wananchi waliofika katika uwanja wa ndege wa Chato.
 • Katika salamu hizo, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Museveni kwa kuja kumtembelea na kuzungumza nae na amebainisha kuwa ziara hiyo inazidi kudhihirisha uhusiano mzuri, wa kidugu, kijirani na kirafiki uliopo kati ya Tanzania na Uganda na kwamba Serikali ya Tanzania itahakikisha uhusiano huo unakuzwa na kuimarishwa zaidi.
MM 3-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na mgeni wake Rais wa Uganda Yoweri Museveni wakati wakipita kwenye Gadi ya Heshma iliyoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ, mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Chato mkoani Geita.
 • Mhe. Rais Magufuli amemuelezea Mhe. Rais Museveni kuwa mmoja wa wanafunzi wazuri wa Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere kutokana na kutambua juhudi kubwa alizozifanya katika kuzisaidia nchi nyingi za Afrika kupigania ukombozi na kuondoa utawala wa mabavu ikiwemo Uganda, na pia kwa maono yake ya kutaka nchi za Afrika Mashariki na Afrika nzima kujielekeza katika kujenga maendeleo na ustawi wa jamii.
MM 4-01
Rais wa Jamhuri ya wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Uganda Yoweri Museveni wakati wakiangalia vikundi mbalimbali vya Ngoma na Kwaya mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Chato mkoani Geita.
 • Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Museveni kwa misaada aliyoitoa kwa Tanzania wakati Mkoa wa Kagera ulipokumbwa na tetemeko la ardhi, ajali ya kivuko cha MV Nyerere na matibabu kwa Mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere alipokuwa nchini Uganda hivi karibuni.
 • Aidha, amemshukuru kwa kufanikisha mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la kuanzia Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania ambalo kwa asilimia 75 ya kilometa zake 1,442 linapita Tanzania, na kubainisha kuwa Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano wa kuhakikisha mradi huo wenye thamani ya takribani shilingi Trilioni 8 unafanikiwa.
MM 5-01
Rais wa Jamhuri ya wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Uganda Yoweri Museveni wakati wakiangalia vikundi mbalimbali vya Ngoma na Kwaya mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Chato mkoani Geita.
 • Pamoja na shukrani hizo, Mhe. Rais Magufuli amesema licha kuongezeka kwa biashara kati ya Tanzania na Uganda kutoka shilingi Bilioni 178.2 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi Bilioni 358.7 mwaka 2018 bado nchi hizo zina fursa nyingi kukuza uchumi kupitia uhusiano wake mzuri.
MM 11-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Uganda Yoweri Museveni wakati waliupokuwa wakiwasalimia wananchi wa Njiapanda Chato mkoani Geita.
 • Amesema katika kufungua fursa zaidi Tanzania imeimarisha bandari ya Dar es Salaam ambayo katika mwaka 2018 ilipitisha mizigo ya Uganda kiasi cha tani 188,591, inajenga meli mpya katika ziwa Victoria na kukarabati meli nyingine 5, imefufua njia ya reli na meli ya kuvusha mabehewa ya treni (MV Umoja) kati ya bandari ya Mwanza na Port Bell nchini Uganda, inashirikiana na Uganda kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme wa Murongo-Kikagati na imeanzisha hifadhi 3 za Taifa katika ukanda wa Kaskazini Magharibi ambazo ni Burigi-Chato, Ibanda-Kyerwa na Rumanyika-Karagwe ili kuimarisha utalii katika eneo hilo.
MM 6-01
Rais wa Jamhuri ya wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Uganda Yoweri Museveni wakati wakiangalia vikundi mbalimbali vya Ngoma na Kwaya mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Chato mkoani Geita.
 • Katika salamu zake, Mhe. Rais Museveni amesema kuja kwake Tanzania ni kama anakuja kufanya Hija kutokana na kutambua mchango mkubwa wa Tanzania wakati wa uongozi wa Hayati Mwl. Nyerere aliyezisaidia nchi nyingi za Afrika kupata uhuru na kuondokana na utawala wa mabavu ambapo yeye na wapigania uhuru wengine Afrika walipata hifadhi na mafunzo Jijini Dar es Salaam.
 • Mhe. Rais Museveni amesema baada ya kupatikana kwa uhuru na ukombozi wa Mataifa ya Afrika jukumu kubwa kwa sasa ni kujielekeza katika maendeleo ya pamoja, maendeleo ya mtu mmoja mmoja na kutengeneza ajira kwa watu ili wapate kipato cha kuwafaa katika Maisha yao.
MM 7-01
Rais wa Uganda Yoweri Museveni akizungumza na Wananchi wa Chato mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Chato mkoani Geita.
 • Amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railway – SGR), ujenzi wa viwanja vya ndege ukiwemo uwanja wa ndege wa Chato, ujenzi wa barabara na usimamizi mzuri wa maliasili utakaosaidia kuchochea uchumi.
MM 8-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na mgeni wake Rais wa Uganda Yoweri Museveni mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Chato mkoani Geita.
 • Baada ya kusalimiana na wananchi, Mhe. Rais Museveni akiwa na mwenyeji wake, Mhe. Rais Magufuli amemjulia hali Mama wa Mhe. Rais Magufuli, Bibi Susana Magufuli ambaye baada ya kupatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete anaendelea na matibabu hayo akiwa nyumbani katika Kijiji cha Mlimani, Wilayani Chato na kisha viongozi hao wamefanya mazungumzo ya faragha.
 • Baada ya mazungumzo hayo viongozi hao wamesema wamekubaliana kukamilishwa kwa masuala machache hasa yahusuyo kodi katika utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta la Hoima – Tanga na kwamba mradi huo utaanza kutekelezwa hivi karibuni.
MM 9-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Uganda Yoweri Museveni kabla ya kuanza mazungumzo yao Chato mkoani Geita. PICHA NA IKULU
 • “Namshukuru sana Mhe. Rais Museveni kwa kuja kunitembelea hapa Chato, ametoka Angola moja kwa moja hadi hapa Chato na amemuona Mama yangu ambaye ni mgonjwa, huu ni upendo wa pekee, lakini zaidi kwa namna anavyomuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwl. Nyerere na anavyoipenda Tanzania, nataka kumhakikishia kuwa Tanzania itahakikisha uhusiano huu na ndugu zetu Waganda unadumishwa” amesema Mhe. Rais Magufuli.
MM 10-01
Baadhi ya Wananchi wa Chato waliojitokeza katika mapokezi ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni Chato mkoani Geita.
 • Kabla ya kuwaaga wananchi wa Chato katika uwanja wa ndege wa Chato  na kurejea nchini Uganda, Mhe. Rais Museveni ameahidi kujenga jengo la vyumba 7 vya madarasa katika shule ya msingi Nyamilezi wilayani humo.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Ad

Chato

13 Julai, 2019

Ad

Unaweza kuangalia pia

LIVE: UZINDUZI WA MAJENGO YA OFISI YA MANISPAA NA MKUU WA WILAYA KIGAMBONI JIJINI DSM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11, Febuari, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.