Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Mjini Dodoma (DUWASA) imejipa siku 100 za kutatua kero ya maji na hivyo kupunguza adha ya ukosefu wa maji iliyopo kwa wananachi katika maeneo mbalimbali wanayoyahudumia.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwa katika ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba kwa ajili ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi ya maji,Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA mhadisi Aron Joseph amesema kwa sasa uhaba wa maji uliopo ni lita Milioni 37 kwa siku.
“Katika kuhakikisha tunapunguza upungufu huo tayari tunachimba visima 10 katika maeneo mbalimbali ikiwemo Ihumwa na Zuzu,lengo letu katika siku hizi 100 tulizojipa tufanye kazi na wananchi wa Dodoma waone matokeo,”alisisitiza.
Amesema katika visima hivyo 10 wanavyochimba pembezoni mwa mji lengo lao ni kuhakikisha ndani ya mwezi huu wa kwanza viwe vimekamilika ili kazi ibaki kwenye kuviendeleza.
“Shughuli tunayoifanya ina lenga kupunguza upungufu kwa maji uliopo wa lita Milioni 37 kwa siku,ambapo kupitia visima hivi tutapata maji lita Milioni 21 hadi 28 kwa siku na hivyo tutasaidia kupunguza uhaba wa maji Dodoma,”aliongeza.
Aidha amesema kupitia chanzo kikuu cha maji cha Mzakwe wanachimba visima vya maji vitatu ambavyo kila kimoja kitatoa maji sio chini ya laki 4 kwa saa kwa hiyo kwa vyote watapata maji sio chini ya lita Milioni 1.2 kwa saa.
Mhandisi Joseph ametaja mikakati mingine wanayoifanya ni kufufua visima vya maji vilivyotelekezwa ambavyo kufanya kazi kwake kutasaidia ongezeko la huduma ya maji kwa wananchi.
“Mpaka sasa tumeshavitambua visima 11 katikati ya mji,na dhamira yetu ni kuvifufua visima hivyo vya zamani ili visaidie kutoa huduma ya maji kwa wananchi na hivyo kupunguza upungufu wa maji uliopo,”alisema Mhandisi huyo.