TUMIENI UMEME KUANZISHA MIRADI YA MAENDELEO – DKT. KALEMANI

  • Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewaasa wananchi wa Kitongoji cha Mwamagili, Wilaya ya Chato, mkoani Geita kutumia umeme aliowawashia rasmi jana, Juni 30, 2019 kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
KL
Sehemu ya umati wa wananchi wa kitongoji cha Mwamagili wilayani Chato, wakishuhudia zoezi la kuwashwa rasmi umeme katika eneo hilo. Zoezi hilo lilifanywa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), Juni 30, 2019.

 

  • Akizungumza na wananchi hao muda mfupi kabla ya kuwasha umeme katika nyumba ya mkazi wa kitongoji hicho, Kashonele Kagodoro, Dkt. Kalemani aliwaambia endapo watautumia ipasavyo, hali zao za maisha zitaboreka zaidi.
  • “Umeme huu siyo kwa ajili ya kuwasha taa peke yake. Anzisheni miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo mashine za kukoboa na kusaga nafaka, saluni za kike na kiume na miradi mingine mbalimbali ili kuinua kipato chenu hivyo kuboresha maisha yenu.”
  • Aidha, Waziri Kalemani ambaye pia ni Mbunge wa eneo hilo (Chato), aligawa vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) kwa nyumba zote 38 za kitongoji hicho, ambazo zilikuwa bado hazijaunganishiwa umeme ikiwa ni sehemu ya kuwahamasisha wananchi husika kulipia gharama ndogo ya shilingi 27,000 tu ili waunganishiwe nishati hiyo.
WATAALAM
Viongozi na wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza na wananchi wa kitongoji cha Mwamagili, wilayani Chato, muda mfupi kabla ya kuwasha rasmi umeme katika eneo hilo, Juni 30, 2019 akiwa katika ziara ya kazi.
  • “Kwa kutumia kifaa hiki cha UMETA, mtaepuka gharama za kutandaza nyaya katika nyumba zenu. Niwaombe na kuwahamasisha muendelee kulipia kwa sababu bei ya kuunganishiwa umeme ni ndogo sana; shilingi 27,000 tu,” asisitiza Waziri.
  • Katika hatua nyingine, Waziri amelipia gharama za kuunganisha umeme katika Kanisa lililopo eneo hilo, ambayo pia ni sehemu ya kuhamasisha viongozi wa taasisi mbalimbali za umma kulipia gharama za umeme ili ziunganishwe.
  • Wananchi kadhaa waliopata fursa ya kueleza maoni yao mbele ya Waziri Kalemani, walipongeza jitihada za Serikali katika kuwapelekea nishati ya umeme.
  • “Hii ni ndoto kwangu. Sikutegemea. Tangu nizaliwe nilikuwa nikiona umeme maeneo ya mijini nilikowahi kutembelea. Sikuwahi kuwaza kuwa iko siku umeme utawashwa kijijini kwetu, tena katika nyumba yangu,” alisema Kagodolo.
  • Waziri Kalemani yuko Chato kwa ziara ya kazi.Na Veronica Simba – Chato
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *