- Manispaa ya Tabora itaanza kupata maji safi na salama wakati wote baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji toka Ziwa Victoria utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 600.
- Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Tabora (TUWASA), Mhandisi Mkama Bwire ameeleza hayo kwa Maafisa wa Idara ya Habari (MAELEZO) walipofanya ziara mkoani humo hivi karibuni.
- “Tunamshukuru sana Rais John Pombe Magufuli kwa utekelezaji wa mradi huu wa maji ambao utakuwa mkombozi kwa Manispaa ya Tabora na maeneo mengine ya mkoa wetu ikiwemo Nzega na Igunga,”anasema Mhandisi Bwire.
- Serikali inataka ifikapo Juni 2020, upatikanaji wa maji safi na salama maeneo ya mijini ufikie asilimia 95, lakini Manispaa ya Tabora imejipanga kuwafikishia wananchi wake huduma hiyo kwa asilimia 100.
- Kwa mujibu wa Mhandisi Bwire, upatikanaji wa maji safi na salama katika kata 20 zinazopata huduma hiyo, ni asilimia 84 tu. Hivyo kuna kila sababu ya kukamilisha mradi huo mapema iwezekanavyo na kufanya upatikanaji wa huduma hiyo kwa asilimia 100 na kwa kata zote za Manispaa ya Tabora.
- Mhandisi Bwire anasema upatikanaji wa maji safi na salama utaongeza na kuchochea shughuli za kiuchumi kwani muda mwingi uliokuwa ukipotea kwa watu kufuata maji zaidi ya kilomita 5 kwa sasa utatumika kwa shughuli za kiuchumi.
- Serikali ya Awamu ya Tano inayolenga kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda, inatekeleza azma hiyo kwa kuwapatia wananchi maji ya uhakika ambayo pia ni kiungo muhimu kwa ujenzi wa viwanda, hivyo Mhandisi Bwire anatumia fursa hiyo kuwaalika wawekezaji kuwekeza katika Mkoa wa Tabora kwani maji ambayo yalikuwa ni kikwazo cha uwekezaji sasa yatapatikana kwa uhakika.
- “Natoa wito kwa wawekezaji hasa kwenye viwanda waje Tabora kwa wingi ili wawekeze kwani maji yatakuwepo ya kutosha kwa muda wa saa 24,”anasema Bwire.
- Akizungumzia Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Komanya Kitwala anasema kuwa mradi huu utafanya uhaba wa maji Mkoa wa Tabora kuwa historia na utasaidia katika kukuza uchumi wa mkoa huo.
- “Tunapongeza juhudi za dhati za Jemedari wetu Mkuu, Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutekeleza Ilani ya Chama Tawala kwa vitendo, nasi wasaidizi wake tutahakikisha miradi mikubwa ya maendeleo hasa ya maji, elimu, miundombinu na afya tunaisimamia kikamilifu ili wananchi wafaidi matunda ya Serikali yao,”anasema Komanya.
- Naye Mkazi wa Manispaa ya Tabora Anicet Masanja anasema kuwa upatikanji wa maji utarahisisha hata kwenye shughuli za kilimo cha mbogamboga na matunda pia na ufagaji.
- “Tutalima mbogamboga na kujipatia kipato pasipo kutegemea mvua kwani tutakuwa na maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, tutafuga kwa sababu tutakuwa na maji ya uhakika kwa ajili ya kunyweshea mifugo yetu,”anasema Masanja. Na Jonas Kamaleki-MAELEZO
Ad