KIVUKO CHA MV. KITUNDA KIMEONDOA USUMBUFU WA USAFIRI KWA WAKAZI WA LINDI

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amepewa pongezi na Wakazi wa Mkoa wa Lindi kwa kuwaletea huduma ya kivuko cha MV Kitunda kinachofanya safari zake kutoka Lindi kwenda ng’ambo ya pili katika eneo la Kitunda.
  • Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni wakati Maafisa Habari wa Idara ya Habari – MAELEZO walipotembelea eneo la feri ambapo kivuko hicho kinafanyia kazi ili kujionea utendaji kazi wa kivuko hicho.
  • Mfanyabiashara na mkazi wa Kitunda, Yusuph Yahya amesema kuwa kabla ya kivuko hicho biashara zilikuwa ngumu kwa sababu uvushaji wa mizigo haukuwa rahisi pia gharama na muda uliokuwa ukitumika kuvusha mizigo hiyo ni kubwa hivyo muda mwingine wafanyabiashara walikuwa wanapata hasara kutokana na mizigo yao kuharibikia njiani wakati wa usafirishaji.
  • “Kwa kweli tunamshukuru sana Rais wetu Magufuli kwa kutuletea kivuko hiki kwani mwanzoni tulikuwa tunatumia usafiri wa boti ndogo ndogo hata magari ilikuwa shida kuyavusha lakini kwa sasa usafiri ni salama biashara zimekuwa zikifanyika kwa urahisi hata gharama za usafirishaji zimeshuka, zamani mzigo mdogo tu unasafirsha zaidi ya shilingi 2000 hadi 3000 lakini sasahivi tunavusha mzigo mdogo kuazia shilingi 1000,” alisema Yahya.
MV 2-01
Kivuko cha MV Kitunda kinachofanya kazi kati ya kuvusha watu kutoka Lindi mjini hadi Kitunda kikiwa na uwezo wa wa kubeba mizigo tani 50, abiria 100, magari madogo 6 makubwa mawili. Kabla ya uwepo wa Kivuko hiki wakazi wa Kitunda walikuwa wanatumia mitumbwi kuvuka upande wa pili. Kivuko hiki kimepelekwa Mkoani Lindi kikitokea Tanga kwa amelekezo ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni kutatua kero ya wakazi wa Kitunda na maeneo mengine ya Lindi.
  • Naye Mkazi wa Manispaa ya Lindi, Shakira Nandonde amesema kuwa kivuko hicho kimewaondolea adha ya usafiri hasa kwa wanawake, watoto na walemavu kwa sababu boti zilikuwa zikipaki mbali na nchi kavu hivyo ilikuwa ni changamoto kuufikia usafiri huo pia kwa wagonjwa ilikuwa changamoto kuwatoa Kitunda kuwaleta Lindi Mjini ambako ndio kuna matibabu makubwa.
  • Mkazi mwingine wa Kitunda, Said Omary ameishukuru Serikali kwa ujio wa kivuko hicho kwani kimepunguza gharama za usafiri kutoka shilingi 500 malipo ya usafiri wa boti mpaka shilingi 300 kwa usafiri wa kivuko pia kivuko hicho kimesaidia kupanua mji wa Kitunda kwani kwa sasa watu wameanza kujenga na wengine wameanza kulima katika maeneo hayo.
  • “Sina cha kusema zaidi ya kuipongeza Serikali na Rais wetu Magufuli ila tunaomba muda uliowekwa wa mwisho saa 12 jioni kwa siku uongezwe ili shughuli zingine ziendelee pia tunaomba kivuko hiki kizidi kuboreshwa ili usafiri uwe wa uhakika,” alisema Omary.
  • Kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba tani 50 kimeanza kufanya kazi Machi,2018, kinabeba abiria 100, magari madogo 6 pamoja na magari makubwa mawili kwa kila safari moja na kwa siku kivuko hicho.Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Ad

Unaweza kuangalia pia

SERIKALI INATARAJIA KUJENGA MINARA 5 YA MAWASILIANO WILAYANI MAFIA

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mh. Injinia Atashasta Nditiye (Mb.) amezindua mnara wa Mawasiliano …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.