VIWANDA VYOTE NCHINI SASA KUWA NA TRANSFOMA ZAO

 • Serikali imetoa agizo kwa mameneja wote wa mikoa wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha viwanda vyote nchini vinafungiwa Transfoma mahsusi kwa matumizi ya viwanda pekee pasipo kuchanganya na matumizi ya wananchi.
 • Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alitoa agizo hilo jana, Julai 17, 2019 akiwa katika ziara ya kazi mkoani Kagera.
 • Akizungumza na Uongozi wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), mkoani humo, mara baada ya kukagua Transfoma mpya iliyofungwa maalumu kwa matumizi ya Shirika hilo; Dkt. Kalemani alisema hatua hiyo itasaidia kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa viwanda hivyo kuviwezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
 • “Wenye viwanda wawe na Transfoma zao, wasichangie matumizi na wananchi. Mwananchi akiunguza kwake anaathiri Kiwanda pia maana umeme utakosekana kote hivyo uzalishaji unasimama. Haifai.”
MM 1-01
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (mwenye miwani) na Ujumbe wake, akizungumza na mwakilishi wa Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) mkoani Kagera, Justin Mrenga (kulia), alipotembelea Taasisi hiyo kukagua uunganishwaji wa umeme, akiwa katika ziara ya kazi, Julai 17, 2019
 • Vilevile, Waziri aliwaagiza mameneja hao nchi nzima kuhakikisha wanabadilisha miundombinu yote ya umeme ambayo ni mibovu katika maeneo yao mathalani Transfoma, Nguzo, Nyaya na Mita ili kuwaondolea wananchi kero za kukatika kwa umeme mara kwa mara.
 • “Meneja yeyote ambaye eneo lake litabainika kuwa na Transfoma iliyoungua au kuharibika kwa kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja na hajafanya jitihada yoyote kutatua, Mkurugenzi Mtendaji mchukulie hatua maana ni hasara kwa Shirika,” aliagiza Waziri.
 • Akifafanua zaidi, alisema miundombinu iliyoharibika isiporekebishwa kwa wakati, husababisha Shirika kupoteza mapato hivyo kuitia hasara Serikali.
 • Akisisitiza kuhusu agizo hilo, Waziri Kalemani alibainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati, imetenga fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo na urekebishaji wa miundombinu mbalimbali ya umeme kwa maeneo yote nchini, hivyo hakuna sababu ya kusuasua katika kutekeleza zoezi hilo.
 • “Mathalani, kwa Mkoa huu wa Kagera, tumetenga jumla ya shilingi bilioni 9.2 kwa mwaka huu kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya umeme,” alibainisha.
 • Katika ziara hiyo, Waziri alitembelea na kukagua uunganishwaji umeme katika Taasisi ya SIDO eneo la Rwamishenye na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA) Tawi la Bulugo wilayani Bukoba, ambapo alikiri kufurahishwa na utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa awali kwa uongozi wa TANESCO, kuzifungia Taasisi hizo Transfoma.
 • Waziri aliambatana na viongozi pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka Wizarani, TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).Na Veronica Simba – Kagera
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *